BERLIN,UJERUMANI

UJERUMANI imewarudisha nyumbani wanawake watatu pamoja na watoto 12 kutoka katika kambi za wakimbizi kaskazini mashariki mwa Syria.

Gazeti la kila wiki la Bild am Sontag,liliripoti kwamba wanawake wote watatu waliondoka Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni kwa ajili ya kwenda kujiunga na Kundi la Dola la Kiislamu.

Gazeti limetaja majina ya watu hao kama Merve A, Yasmin A na Leonora M. Vilevile ofisi ya mwendesha mashitaka ya Ujerumani ilimtaja raia wa Ujerumani kwa jina la Leonora M, akiwa miongoni mwa majina yaliyotajwa na gazeti la Bild, kwamba alikamatwa alipowasili katika uwanja wa ndege wa Frankfurt.

Alisema ni mwanachama wa kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, na kudaiwa kushiriki kufanya matendo ya uhalifu.