MAPUTO, MSUMBIJI

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICEF limesema takribani watoto 250,000 wamekimbia makaazi yao kutokana na hujuma za kigaidi zinazoendelea kwenye jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji na sasa wako hatarini kupata magonjwa ya kuambukiza kwa kuwa msimu wa mvua unaanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietter Fore alinukuliwa katika taarifa ya UNICEF akisema kuwa katika kipindi kisichozidi miaka miwili,watoto na familia zao huko Cabo Delgado walikumbwa na kimbunga,mafuriko,ukame,machungu ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na COVID-19 na sasa mapigano.

UNICEF ilisema watoto wawili kati ya watano jimboni Cabo Delgado wana utapiamlo na hiyo imechochewa zaidi na majanga yatokanayo na hali ya hewa na mapigano.

Ukosefu wa chakula na njaa ndio matokeo ya hali hizo tete jimboni humo na sasa watoto wengi zaidi wanabainika kuwa na utapiamlo uliokithiri.

Eneo la Cabo Delgado lenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi limekuwa likilengwa na magaidi tangu mwaka 2017.

Mwezi uliopita, Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM lilitangaza kuwa, makumi ya maelfu ya wananchi wanaendelea kukimbia ghasia jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji huku serikali na wadau wa kibinadamu wakishindwa kukidhi mahitaji ya watu hao ya malazi, chakula na misaada mengine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea wasiwasi wake juu ya janga linaloendelea huko Cabo Delgado ikiwemo watu waliojihami kuua wananchi kwa kuwakata vichwa na hata kubaka wanawake na watoto, na hivyo kutoa wito wa kutaka mzozo huo utatuliwe.

Nchi jirani za Tanzania na Zimbabwe zinaisaidia serikali ya Msumbiji kukabiliana na wimbi la ugaidi katika eneo hilo.