MOSCOW,URUSI

URUSI imemtaka mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa serikali Alexei Navalny, kurejea nyumbani mara moja akitokea Ujerumani.

Mamlaka ya magereza ya Urusi, imetoa muda wa mwisho wa hadi jana asubuhi kwa mwanasiasa huyo kuripoti mjini Moscow au kufungwa jela ikiwa atarudi baada ya tarehe hiyo ya mwisho kupita.

Navalny ambaye ni mkosoaji mkubwa wa rais Vladmir Putin, alikimbizwa kwa dharura nchini Ujerumani kwa matibabu mwezi agosti, baada ya kulishwa sumu katika hatua ambayo mataifa ya magharibi yanasema ilikuwa ni jaribio la mauaji.

Urusi inasisitiza kwamba hakuna ushahidi mwanasiasa huyo kupewa sumu na inakataa madai ya kuhusika.

Mamlaka ya Magereza imemshutumu Navalny kwa kukiuka masharti ya hukumu ya kifungo ambacho bado anahudumia kutoka mwaka 2014. Urusi ilidai kwamba Navalny anaweza kurejea nyumbani kama raia wengine.