NA JUMA KHATIB SHAALI (JKU)

MKUU wa Zoni ya Kusini Unguja wa Jesshi la Kujenga Uchumi, Luteni Kanali, Khadija Ahmada Rai, aliwataka vijana wa kujitolea wa JKU kuyatumia vyema Mafunzo waliyoyapata ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Aliyasema hayo wakati alipokua akifunga mafunzo ya vijana hao wa mkupuo wa 065 zoni Kusini katika kambi ya JKU Bambi Kim, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kutokana na elimu kubwa walioipata ya kilimo, ufugaji, Biashara pamoja na ujasiriamali ni vyema kuunda vikundi mbali mbali vya ushirika kwa lengo la kujiajiri na kuondokana na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kutoka Serikalini.

Hata hivyo, aliwataka vijana hao kuwa walimu kwa wengine katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili kuendeleza amani na utulivu nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa kikosi cha JKU Bambi, Kim Meja Alawi Haji Hamadi, alisema kuwa jumla ya vijana 345 wamehitimu mafunzo hayo na kuiomba Serikali kuwaangalia vijana hao katika suala zima la ajira.

Aidha, alitaja baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na uchache wa mabwalo,Vitanda na Magodoro ya kulalia vijana, upungufu wa Wakufunzi, pamoja na ukosefu wa Yunifomu maalumu za kuendeshea mafunzo.

Akisoma Risala kwa niaba ya vijana wenzake, Sabrina Said Abdalla, alisema watahakikisha wanayafanyia kazi mafunzo walioyapata sambamba na kudumisha nidhamu na uzalendo wa nchi yao.