NA MADINA ISSA

VIJANA wajasiriamali nchini wametakiwa kuzitumia fursa za mikopo zilizowekwa na taasisi za kifedha pamoja na mifuko mbalimbali ya hifadhi na uwezeshaji ili kusudi waweze kufikia lengo la ujasiriamali wao.

Afisa mikopo kutoka mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, Safia Mwinyi, aliyasema hayo katika mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wa mkoa huo wa kuweza kuzitumia fursa hizo yaliyofanyika katika ukumbi wa walimu Dunga mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema azma ya serikali ni kuhakikisha wajasiriamali wanawezeshwa ili kuipunguzia serikali mzigo wa vijana wengi wanasubiri ajira kutoka serikalini.

Aidha alisema kuwa mfuko huo umeandaa mikopo kwa ajili ya wajasiriamali ili waweze kufanikisha matarajio yao huku akisema mfuko umeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 ambapo asilimia 76 ni kwa vijana.

Ka upande wake Mkuu wa mfuko wa uchangiaji wa hiari wa ZSSF, Rajab Ali Machano, alisema mfuko wa uchangiaji wa hiari ni mfuko ulioanzishwa kwa lengo la kuwakomboa wananchi ambao hamo katika sekta rasmi haswa wajasiriamali ili uweze kuwasaidia pale wanapopata matatizo pamoja na wanapofikia uzeeni.

Hivyo, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiunga na mfuko huo ili kuweza kuwasaidia katika kufanya shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo.

Nae Ali Shaibu Mussa kutoka benk ya NMB alisema benki ya NMB imeshatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijiji 75 na kuwapatia elimu wananchi 13 elfu na kuwapatia mikopo wajasiriamali hao ili waweze kufikia malengo ya serikali katika kuwawezesha wajasiriamali.

Sambamba na hayo, aliwataka vijana kuachana na dhana potofu za kusema hakuna fursa huku akiwasisitiza vijana kukaa pamoja na kubuni njia zitakazowasaidia kujikwamua katika wimbi la umasikini.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema watayatumia vyema mafunzo hayo kwa kuhakikisha fursa zitakazoibuliwa watazitumia kwa maslahi ya vijana wote.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na jumuiya ya habari dhidi ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya Zanzibar ZAIADA ambapo Taasisi mbalimbali za fedha na mifuko ya hifadhi na uwezeshaji wananchi kiuchumi zilifungua milango ya fursa kwa wajasiriamali hao.

Wakati huohuo Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Wilaya Ya Kati limetakiwa kusimamia kikamilifu upatikanaji wa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya ushirika vya akinamama viliyomo wilayani humo ili viweze kuzalisha bidhaa zenye ubora.