HAKI na wajibu ni vitu muhimu vya kuzingatiwa katika mustakabali mzima wa maisha ya kila siku ya mwanadamu iwe ndani ya familia, katika maeneo ya kazi nakadhalika.

Ukweli ni kwamba iwapo haki na wajibu ambapo wakati mwengine huhesabiwa kama watoto pacha, yatachukua nafasi yake inavyostahiki uwezekano mkubwa wa kuimarika kwa familia bora na utendaji kazi uliotukuka.

Lakini kinyume chake hasa katika maeneo ya kazi kama mtumishi atakuwa anadai haki pasi na kutekeleza wajibu wake itegemewe kuibuka kwa mgogoro, kujengewa chuki na lawama.

Kwa upande mwengine wa shilingi ikitokezea watu wanatekeleza wajibu wao lakini haki imekuwa ngumu kuipata, hapo nao lazima mambo hayatakuwa sawa.

Suala la haki na wajibu kama tulivyoliita kuwa ni watoto pacha, ni muhimu sana kwa mustakbali wa taifa ambapo ipo haja ya kusimamiwa ipasavyo ili kuondosha manung’uniko na lawama.

Inapotokezea watoto pacha hao wakitenganishwa kwa kukosekana usimamizi kwa kiongozi aliyepwa dhamana kwenye taasisi ni vigumu kwa watendaji kuwepo kwa upendo baina yao na badala yake chuki na hasama ndiyo yatakuwa maisha yao.

Katika hali kama hiyo kwenye taasisi pasitarajiwe kupatikana kwa ufanisi kwani kutakuwa na ushindani baina ya viongozi na watendaji kama hiyo haitoshi uharibufu wa mali za umma nao utarajiwe kujitokeza.

Kama tulivyosema Kwamba haki na wajibu ni mambo yanayokwenda sambamba, hivyo kila upande ni lazima kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wake.

Kwa mfano ikitokea kiongozi anayesimamia watu kwa upendeleo na matakwa binafsi bila ya shaka hastahiki kuvumiliwa kwani ni miongoni mwa watu wanaorejesha juhudi za watendaji sambamba na kudumaza mipango ya serikali iliyojiwekea.

Katika taasisi zetu, watendaji wanaelewa fika yupi mfanyakazi anayechapa kazi na kuwajibika inavyostahiki na yupi anayetegea na kufanyakazi kiujanja ujanja.

Ukweli hatukusuduii kumnyoshea kidole kiongozi au mtendaji yoyote, isipokuwa tukiwa kama waumini tumechukua fursa hii kuwatanabahisha viongozi kuacha tabia hiyo.

Tunasema hivyo kwa sababu ya kukumbusha kwamba endapo ukishindwa kuwapa au kuwasimamia haki za wafanyakazi waliochini yako waliotekeleza wajibu wao inavyotakiwa, ipo siku watakwenda kudai na bila shaka siku hiyo hutakuwa na uwezo wa kuwalipa.

Lakini kulitanabahisha kundi kubwa la watendaji wasiowajibika ambapo kwa kawaida hufanyakazi kiunjanja kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao inavyostahiki, kwamba kazi ni ibada na kipato cha kazi yako kitaulizwa baada ya maisha ya duniani.

Ewe mtumishi, kama unatabia ya kushindwa kuwajibika badala yake unadai haki hata ile usiyostahiki, tambua kuwa unajitengezea masuali mengi ifikapo siku kubwa ambayo utasimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hivyo, viongozi, watendaji na watumishi wasiotekeleza wajibu wao vyema, huu ni wakati wa kujirekebisha na ni vyema kuanzia tukajihukumu wenyewe huku tukijiuliza kuwa nini serikali inavyonifanyia, lakini pia kujiuliza nini serikali naifanyia.

Kuna haja ya viongozi kuwapa motisha watendaji wao wanaonekana kutekeleza majukumu yao jambo ambalo litawapa ari na mori wale wasiotekeleza wajibu wao kazini.

Hivyo ni vyema kila aliekabidhiwa dhamana atambue suala la kusimamia kwa umakini haki na wajibu ni jambo la msingi na lina umuhimu wake kwani yapo maisha baada ya uongozi.