MINSK,BELARUS

WATU wapatao 100 wametiwa mbaroni na polisi katika mji mkuu wa Belarus, Minsk, wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

Kituo cha kutetea haki za binadamu cha Viasna kilichapisha majina ya watu 141 waliokamatwa na polisi mjini Minsk na katika miji mengine kulikofanyika maandamano hayo.

Waandamanaji waliamua kutumia mbinu mpya ya kukusanyika katika makundi madogo madogo kote nchini humo, ili iwe vigumu kulengwa kwa wakati mmoja na vikosi vya usalama.

Maandamano hayo yaliyodumu kwa miezi minne sasa, yalizuka baada ya Rais Alexander Lukashenko kuchaguliwa kwa muhula mwengine madarakani katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Lukashenko alimshinda mpinzani wake Sviatlana Tsikhanouskaya ambaye alikataa kuyatambua matokeo hayo akidai uchaguzi ulikuwa na udanganyifu.