NA HANIFA SALIM
OFISA Mdhamini Tume ya Mipango Pemba, Dadi Faki Dadi, amewaasa waandishi wa habari na watafiti kuzingatia mbinu watakazozipata katika mafunzo ya uandishi wa habari za sayansi teknolojia na ubunifu, ili ziweze kuleta tija kwa jamii.
Alieleza hayo wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari, wahiriri na watafiti juu ya uandishi wa habari za sayansi teknolojia na ubunifu, katika ukumbi wa maabara kuu Wawi Chake Chake.
Aidha alishauri, pamoja na majukumu mengine tume imepewa jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kusambaza taarifa za sayansi teknolojia na ubunifu ili ziweze kutumiwa na Watanzania kwa maendeleo.
Mapema Kamishna wa idara ya mipango na utafiti Zanzibar, Dk. Afua Khalfan Mohamed alisema, wanatoa mafunzo kwa waandishi na wahariri lakini bado kuna changamoto katika uandishi wa habari za utafiti.
“Wanahabari wengi hawana ueledi wa kuandaa
taarifa hizi, na namna
ya kuziwasilisha kwa jamii lakini ukosefu wa taarifa na mahusiano
ya karibu baina ya wanahabari, watafiti na
wabunifu hii imeleta changamoto,”
alisema.
Alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuwaunganisha watafiti na waandishi wa habari ili kusaidia kuondosha kasoro zilizopo baina ya waandishi na watafiti.
Mapema Kaimu Mkurugenzi utawala wa maarifa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia,Dk. Bunini Munyilizu, alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuunganisha kundi moja la wadau hao kisiwani Pemba ili kupeleka taarifa kwa jamii na ushauri kwa serikali.