NA KHAMISUU ABDALLAH

WAANDISHI wa habari wameombwa kuandika habari za kujenga umoja ili kuwaweka wananchi kuwa kitu kimoja na kuifanyia kazi dhana ya maridhiano ya kisasa yaliyofikiwa Zanzibar

Kaimu Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Imane Osmane Duwe, aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari juu ya habari zinazohamasisha amani na utulivu wa kisiasa katika kuimarisha serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema hatua hiyo itasaidia wananchi kushirikiana na kusahau tofauti zao zilizokuwepo kabla ya kuwepo kwa madhiriano ya kisiasa yaliyopelekea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Alisema waandishi wa habari wanaoaminika kama watetezi wa wananchi na wanaweza kuwasemea matatizo yao, hivyo kuwaandikia habari za kuwashajihisha kuwa wamoja zitaleta mafanikio miongoni mwao.

“Vyombo vya habari vina nguvu kubwa kwa jamii na mnaamika kwa asilimia kubwa hivyo ni vyema mkatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi ili kuwafanya wananchi wa Zanzibar wasirudi katika mifarakano bdala yake muwaunganisheili kupiga hatua za maendeleo,” alisema.

Aidha aliwasisitiza wanahabari kuacha kuwa na mihemko ya wanasiasa, badala yake kufuata maadili ya tasnia hiyo kwani wanaweza kuleta matatizo kwao binafsi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo alibainisha kuwa ni jambo la msingi kwa na muhimu kwa waandishi kutathmini taarifa wanapotaka kuandika athari na faida zake kwa jamii baada ya kusikika ili kuepuka nchi kujiingiza kwenye matatizo.

Duwe alisisitiza kuwa kazi iliyopo sasa ni wanahabari kutumia kalamu zao vizuri kwa kufuata maadili ya kazi zao kwa kuondosha makovu na maumivu ili kuona serikali ya umoja wa kitaifa inaendelea kudumu.

“Tumeona kasi ya Rais Dk. Mwinyi, ameonesha dhamira njema ya kuwa na nia thabit ya kuwatumikia wananchi. Nyinyi waandishi mna jukumu la kuisaidia serikali kuibua matatizo yanayoikabili jamii ili yajulikane na kufanyiwa kazi,” alisema.