NEW YORK, MAREKANI

IDADI ya waandishi wa habari waliouawa katika mataifa ya kusini mwa Marekani kwa mwaka 2020 imefikia 23, baada ya mmiliki na mtangazaji wa kituo kimoja cha redio kuuawa nchini Honduras.

Kwa mujibu wa Shirika la Waandishi wa Habari la Marekani, Pedro Arcangel Canellas, anayemiliki Radio Bambi na mtangazaji wa kipindi mashuhuri cha Correo Informativo alipigwa risasi na mwendesha pikipiki mwishoni mwa wiki iliyopita.

Shirika hilo limeitaka serikali ya Honduras kuchunguza tukio hilo, ambalo ni la nne kwa mwaka huu nchini humo.

Mwandishi mwengine wa habari Luis Alonso Alomendares aliuawa mwezi Septemba, mauaji yaliyotanguliwa na yale ya mwandishi German Vallencillo na mpiga picha Jorge Posas mwezi Julai.

Mbali ya Honduras, matukio 19 ya mauaji ya waandishi yalitokea katika mwaka 2020, ambapo 11 waliuawa nchini Mexico, wawili Venezuela, wawili Guatemala, huku Barbados, Brazil, Colombia na Paraguay zikipoteza mwandishi mmoja kila moja.