NA AMEIR KHALID

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini B Rajab Ali Rajab amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuendelezwa michezo katika skuli na vyuo vikuu ili taifa liwe na wachezaji wazuri.

Alitoa kauli hiyo wakati wa kuwapokea wachezaji wa timu ya Baseball na Softball pamoja na timu ya Chuo Kikuu cha Al-Sumait , baada ya timu hizo kuwasili Zanzibar zikitokea Tanzania bara.

Timu za Baseball na Softball za skuli ya Mwanakwerekwe C na Ndijani zilishiriki mashindano ya Baseball Dar Salaam na kushika nafasi ya pili, wakati timu ya chuo kikuu Chukwani ilishiriki mashindano ya vyuo vikuu Tanzania na kutwaa ubingwa huko Dodoma.

Mkuu huyo wa wilaya alisema michezo katika vyuo vikuu na skuli ina umuhimu mkubwa kwani inatoa fursa ya mwanafunzi kupata mafanikio katika, kwani si kila mwanafunzi anafanikiwa maisha kupitia masomo, na wapo baadhi ya watu wamefanikiwa maisha yao kwa michezo.

Alisema timu hizo kupata nafasi ya kwanza na ya pili katika mashindaano walioshiriki ni jambo la faraja kwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi, ambayo inakusudia kuifanya michezo kuwa ni moja ya sehemu zinazotoa ajira nyingi kwa vijana.

Pia alizipongeza kwa kufanikiwa kupata nafasi hizo kwani historia inaonyesha kuwa timu za Zanzibar zinaposhindana na timu za Bara hupata ushindani mkali, hivyo kitendo cha kupata nafasi ya ubingwa na mshindi wa pili na hatua kubwa na yenye mafanikio.

Mapema Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Maktaba Sichana Haji Foum , amesema wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imefarajika sana na matokeo hayo yanadhihirisha kuwa kuna kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya kuvumbua na kuibua vipaji vya vijana.

Mkurugenzi Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu Zanzibar Hassan Khairalla Tawakal, alisema idara yake itahakikisha inaendelea kuvumbua na kulea vipaji vya michezo na Sanaa katika skuli na vyuo, ili Zanzibar iendelea kuwa na wanamichezo na wasanii wenye vipaji.