NA LAILA KEIS

WAFANYABIASHARA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kukata leseni za Biashara zao, ili kwenda sambamba na kasi ya serikali ya kukuza pato la nchi.

Ofisa Mapato Msaidizi Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mohammed Talib, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mombasa mjini Unguja.

Alisema, muamko wa kila mwaka kwa wafanya biashara kukata leseni huwa ni mdogo, hivyo matarajio yao kwa mwaka huu watajitokeza kwa wingi, ili kwenda sambamba na kasi ya Rais ya kuinua uchumi wa nchi kwa haraka.

“Ili kufikia lengo la serikali la kukuza uchumi wa nchi kwa haraka, wafanyabiashara wanatakiwa kuunga mkono ukusanyaji wa mapato kwa kutopuuza suala zima la ukataji wa leseni, zoezi ambalo ni mara moja kwa kila mwaka” alisema.

Aidha, alisema ukusanyaji wa mapato unasaidia katika kuendeleza shughuli na miradi mbalj mbali katika jamii, hivyo kila mfanyabiashara hana budi kujuwa wajibu wake kwa kutodharau sheria za nchi.

Alisema kutokana na muamko wa wafanya biashara kuwa mdogo katika kuchukua fomu za leseni, watendaji wa baraza hilo huchukua hatua ya kutembelea madukani, kwa ajili ya kuwauzia wafanyabiashara fomu hizo.

Sambamba na hilo alisema ili wafanya biashara wajue umuhimu wa kukata leseni, Baraza hilo hutoa mafunzo maalumu kwao, ili washajihike kukusanya mapato kwa ajili ya kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Alifafanua kwa kusema, Baraza lipo katika mchakato wa kutoa fomu za kuchukulia leseni lililoanza Tarehe mosi mwezi huu, ambapo zoezi hilo linaendelea hadi Januari pili kwa ajili ya kusajiliwa, hivyo aliwatala wafanya biashara kutopuuza agizo la serikali.

Akizungumzia ukataji huo wa leseni, mfanyabiashara ya nguo maeneo ya Mchina Mwanzo Khamis Abdallah alisema, kinachowakwamisha baadhi yao kutokata leseni ni ugumu wa biashara kwa baadhi ya siku.

Lakini aliwataka wafanya biashara wenziwe kutodharau agizo hilo, kwani mbali na kuisaidia nchi kukuza pato lake, lakini pia inawasaidia kufanya biashara zao kwa uhuru, bila mvutano wowote baina yao na Baraza la Manispaa.