NA ABOUD MAHMOUD

WAFANYAKAZI wa Shirika la Bandari Zanzibar wameiomba Serikali kwa kushirikiana na  Mkurugenzi Mkuu  kuivunja bodi ya shirika hilo kutokana na utendaji wake kuwa upo kinyume na matarajio ya wafanyakazi katika kuwaletea maendeleo.

Wafanyakazi hao waliyasema hayo wakati walipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Naahat Mohammed Mahfoudh,  katika kikao cha pamoja kilichofanyika kwenye ukumbi wa shirika hilo.

Wafanyakazi hao walisema ipo haja kwa Mkurugenzi huyo mpya kuiangalia kwa kina bodi hiyo kwa madai ya kuwa ipo kwa maslahi yao binafsi na sio kwa wanafanyakazi wala Serikali kwa ujumla.

“Nakuomba Mkurugenzi wetu mpya kuivunja bodi ya shirika la bandari hii haina maslahi kabisa na sisi wao wapo kwa malengo yao binafsi tangu kuundwa kwa bodi hii haijawahi hata siku moja kupita katika Idara hizi kuulizia changamoto tulizokua nazo,”alisema Saleh Yussuf.

Wafanyakazi hao walisema mbali na hilo, lakini wamekua na kero mbali mbali zinazowakabili ikiwemo uchelewashwaji wa posho zao  ambao unachukua muda mrefu kulipwa jambo ambalo linawafanya kufanya kazi kwa unyonge.

Aidha, walimuomba Mkurugenzi huyo kuhakikisha anawapatia njia itakayowasaidia kupata nafasi za kwenda masomoni kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa kazi zao.

“Wafanyakazi tunajituma sana kwa muda mrefu na tatizo jengine linalotukabili ni kucheleweshewa kwa posho zetu hali ambayo inatufanya kufanya kazi tukiwa na unyonge tunakuomba utusaidie kwa hili, lakini pia tunahitaji kwenda kusoma kuongeza ujuzi tunaomba utusaidie ili shirika letu liwe na watendaji wenye ufanisi zaidi,”alisema Tatu Elias,

Nae Mkurugenzi Mkuu huyo, alisema maendeleo ya  shirika hilo hayawezi kuletwa na yeye peke yake bila ya kuwa na mashirikiano ya pamoja baina yake na wafanyakazi.

Hivyo aliwaomba watendaji hao kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja bila ya kuweka ubaguzi wa aina yoyote katika kuliletea maendeleo shirika hilo ambapo amesema kwa kipindi kifupi tayari kumeanza kuonekana mabadiliko.

“Nakuombeni wafanyakazi wenzangu tuzidishe mashirikiano ambayo yatatusaidia kufikia malengo tulioyakusudia katika shirika letu hili, waswahili wanasema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu hivyo naamini kama tutashirikiana tutafanikiwa katika Idara zetu zote zilizokuemo katika shirika,”alisema.

Nahaat alieleza kwamba mashirikiano watakayoyaweka yatalazimisha shirika kutengezwa upya, ili kuweza kupatikana mafanikio, ambapo pia alisema maazimio hayo yatajenga mifumo thabiti ya kiutendaji.