NA ASYA HASSAN

WIZARA ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar imewaomba wajasiriamali na wafanyabiashara mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuwasilisha maombi mapema, ili waweze kupata nafasi ya kushiriki katika tamasha la saba la biashara.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Juma Hassan Reli, alisema hadi hivi sasa kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara hao kutaka kushiriki katika maonesho hayo hivyo ni vyema kwa wale wote wenyenia kujitokeza mapema ili kupata nafasi hiyo.

Alisema tamasha hilo la wafanyabiashara ikiwa ni shamrashamra za kusheherekea miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar linatarajiwa kuanza Januari 4, 2021 katika viwanja vya Maisara wilaya ya Mjini Unguja.

Alifahamisha kwamba tamasha hilo ambalo linatarajiwa kushiriki wajasiriamali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo kutoka ndani nan je ya Tanzania pamoja na taasisi za serikali.

Katibu huyo alifahamisha kwamba kupitia tamasha hilo ni chachu kwa wajasiriamali, wafanyabiashara na taasisi hizo kuweza kutangaza biashara na huduma zao.

Hata hivyo alifahamisha kwamba hadi sasa washiriki 250 tayari washawasilisha maombi yao, hivyo ni vyema kwa wale wote wenyenia ya kushiriki katika tamasha hilo wakawasilisha maombi yao ili kuondosha usumbufu wakati unapofika.

Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo Katibu huyo, alisema maandalizi hayo yashakamilika kwa asilimia kubwa kilichobaki ni kuendelea kupokea maombi kutoka kwa washiriki wengine.

Akizungumzia mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo alisema hadi sasa hawajamjua lakini wanategemea kuwa kiongozi wa juu wa serikali.