NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, amesema hatomvumilia Mkaguzi yoyote atakaetumia vibaya fedha za umma badala yake wazingatie maadili ya kazi na uaminifu kulingana na mabadiliko ya nchi.

Waziri huyo, aliyasema hayo ofisini kwake Vuga wakati alipokutana na wakaguzi wa ndani wa wizara hiyo juu ya kutumia matumizi vizuri ya fedha pamoja na rasilimali watu kwa lengo la kujua ufanisi wa kazi zao.

Alisema hivi sasa nchi imekuwa na mfumo mpya wa kasi ya upatikanaji maendeleo, hivyo ni vyema kusimamia wajibu wao ili kuona lengo lililokusudiwa linafikiwa.

Aidha, aliwataka wasiruhusu kutumika fedha katika matumizi mabaya kwani hali hiyo itapoteza muelekeo wa serikali na kushindwa kupiga hatua katika mfumo mzima wa upatikanaji wa maendeleo endelevu nchini humo.

“Kama kuna mkaguzi wa ndani bado ana mambo yale yale ya zamani basi wakati ndio huu wa kujirekebisha mapema kwani endapo nikimgundua kati yenu hakika sitoweza kumuonea muhali na nitamuadabisha,” alisema.

Waziri huyo alisema kinachoonekana kwa wakaguzi hao ni hofu na muhali, hivyo walitoa wasiwasi na kuwataka kuhakikisha kila mmoja anasimamia vyema sheria inavyoeleza ili kuona mabadiliko chanya yanapatikana.

Waziri huyo alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuleta mabadiliko kwenye rasiliamli fedha na rasilimali watu kwa maslahi ya sasa na baadae.

“Fedha za umma zinapotea ufanisi hauonekani hii ni kutokana na kuwa wengi wao wanatii sheria inayoonesha ishara ya ubadhirifu,” alisema waziri huyo.

Wakaguzi hao walipotakiwa kutoa changamoto zao zinazowakabili, walisema wanahitaji mashirikiano ya pamoja kwa taasisi husika kwani imetajwa kuwa ndio sababu kuu ya kukwamisha malengo yao.

Walisema ili wafanye kazi zao kwa ufanisi wanahitaji kwenda mafunzo nje ya kazi zao ili vitu vyote vinavyowakabili wawe na uwezo wa kuvikagua ipasavyo na badala yake kuacha kabisa kufanyakazi kimazoea.

Aidha, walisema wamekuwa wakifuatilia kwa undani kazi zao lakini cha kusikitisha hazifanyiwi kazi jambo ambalo linawakwamisha katika juhudi zao za kufanyakazi.

“Mimi kama mimi nimeomba vifaa nishaandika barua mara tatu lakini sijapatiwa vifaa na kupelekea ripoti tunazozifanya kuvuja kabla kufikishwa sehemu husika,” alisema Mustafa Daudi kutoka wilaya ya Kusini.

Vikao kama hivyo vitakuwa endelevu wizarani hapo kwa lengo la kujuilishana nini kinaendelea na nini cha kufanya ili kuweza kuwarahisishia ufanyaji wa kazi zao za kila siku.