NA HABIBA ZARALI

WAKULIMA 100 wa mpunga na mboga katika bonde la Mjumbe shehia ya Kangagani Kisiwani Pemba, wanaendelea kunufaika na kilimo hicho baada ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuwajengea bwawa la kuhifadhia maji kwa ajili ya kumwagilia kilimo hicho.

Ujenzi wa bwawa hilo uliogharimu shilingi milioni 89 lengo lake ni kuwasaidia wakulima kulima kilimo cha kisasa kilichofanyiwa utafiti.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika bonde hilo, mkulima Omar Mussa Othman, alisema kabla ya kulima kilimo hicho, alikuwa akipata mazao duni licha ya kazi kubwa aliyokuwa nayo.

Alisema alikuwa akipata polo moja tu la mpunga lakini sasa  anapata polo kumi jambo ambalo ni faraja kubwa kwake.

Mkulima huyo alisema mbegu wanazolima ikiwemo supa India inawaletea faida kubwa tofauti na mbegu zile za zamani ikiwemo ringa na haliuku ambazo uzalishaji wake haukuwa mzuri.

“Utafiti ni jambo moja zuri kwani linatupa uhakika wa mavuno sisi wakulima,” alisema.

Alifahamisha kilimo hicho ni kwa ajili ya kuboresha mpunga wa juu na mboga ambapo mkulima anaweza kulima mara mbili kwa mwaka.

Alieleza kuwa yeye mwenyewe hana shida ya chakula kwa sasa kwani mapolo ya mbunga yanakutana kabla ya kumalizika, hivyo aliwashauri wenzake kuendeleza kilimo hicho ili kujikomboa na umasikini.

Nae mkulima wa mpunga na tungule,  Khamis Zubeir Kassim, alithibitisha kupata faida kubwa ya kilimo hicho ambapo alisema hapo awali alikuwa anasia pishi saba na kupata mpunga kipolo kimoja lakini sasa anasia pishi  tatu tu na anapata mpunga polo kumi.

Alisema ni jambo la faraja kwa COSTECH kuwajengea bwawa ambalo linawasaidia kumwagilia kilimo chao.

Alizitaja changamoto zinazowakumba katika kilimo chao kuwa  ni pamoja na watu kuvua kambare katika bwawa lao pamoja na kuwafungia ng’ombe jambo ambalo linawarejesha nyuma katika juhudi zao.
“Ni vyema wakulima tuuthamini mradi wetu huu kwani unatusaidia kutuondoa katika umasikini na kutuweka katika maisha mazuri,” alisema.
Mtaalamu wa kilimo katika bonde hilo, Bakar Said Saleh alifahamisha, kuwa wanaendelea kuwapa taaluma wakulima hao ili waweze kulima mazao hayo na kupata tija.

Akitaja changamoto zinazowakabili alisema ni pamoja na umasikini kwa wakulima hao pamoja na elimu ndogo licha ya kuwa inatolewa mara kwa
mara.
Akitoa ushauri wake kwa wizara ya kilimo, alisema ni vyema kuweka  mpango maalum wa kutoa elimu zaidi ili wakulima waweze kuimarika zaidi.
Wakizungumza baadhi ya wananchi wa eneo hilo ambao hawajaanza kulima kilimo hicho, walisema walishindwa kufanya hivyo kutokana na hali duni
za maisha yao.

Kilimo cha kitaalamu ambacho tayari kimefanyiwa utafiti kinawakomboa mkulima na unyonge wa umasikini wa chakula.