NA ASYA HASSAN

BAADHI ya wakulima wa Mwani Mkoa wa Kusini Unguja, wameiomba serikali kuwawekea mazingira mazuri katika kilimo hicho, ili waweze kulima katika maji ya kina kirefu.

Wakulima hao, walisema hayo walipokuwa wakipatiwa mafunzo ya kuogelea na usalama kwenye maji pamoja na huduma ya kwanza mafunzo ambayo yanatolewa na Taasisi ya Panje Project.

Walisema hatu hiyo itasaidia kuzalisha rasilimali hiyo katika kiwango kizuri pamoja na kufikiwa kwa uchumi wa buluu.

Wakulima hao walifahamisha kwamba sekta hiyo muhimu katika kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hivyo ni vyema kuwekewa miundombinu imara ili lengo la serikali la kufikiwa kwa uchumi huo liweze kufanikiwa kupitia sekta zote.

Mwenyekiti wa kikundi cha Tunaweza’ ambacho kinajishulisha na kilimo cha mwani pamoja na kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na rasilimali hiyo Mwanaisha Makame Simai, alisema kupatiwa mafunzo hayo ni chachu ya kuwaongezea mbinu na ujuzi wa kilimo hicho.

Alisema mafunzo hayo pia yatawasaidia kuondokana na uzalishaji wa zamani na kuzalisha bidhaa hiyo katika maji ya kina kirefu hali ambayo itasaidia kuongeza motisha katika uzalishaji wao.

“Uchumi wa buluu ni kuweza kuzitumia ipasavyo rasilimali ziliyopo baharini na kuona zinaleta tija kwa watu wote,”alisema.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kuweza kuja na dhana ya uchumi wa buluu, kwani mategemeo yao itaweza kuwanufaisha watu wote.

Meneja wa taasisi ya Panje, Muhammad Suleiman Said, alisema taasisi hiyo imeona ipo haja ya kutoa taaluma hiyo kwa kinamama hao, ili kuwawezesha kufika katika maji ya kina kirefu pamoja na kuwa na usalama katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Meneja huyo alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji na kuchochea kuinua kwa uchumi wa nchi.

Alisema serikali inasisitiza kuimarishwa kwa uchumi wa buluu, hivyo na wao wanaiunga mkono serikali kwa kuwawezesha kina mama hao kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuleta tija hapa nchini.