NA RAHMA JUMA

WAKULIMA kisiwani Pemba wameshauriwa kubadilika kwa kulima kilimo cha kisasa na kutumia mbegu ambazo zimefanyiwa utafiti.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) Pemba, Khatib BakarHaji, baada ya kutembelewa na waandishi wa habari katika shamba liliopo Mbunzini Chake Chake Pemba kwa lengo la kujua faida za kilimo cha kisasa kilichofanyiwa utafiti.

Alisema wakulima watakapotumia mbegu zilizofanyiwa utafiti wataongeza uzalishaji na kuongeza kipato chao.

Mmoja ya wakulima wa zao la muhogo na viazi vitamu, Fatma Bakar Hamad, alisema kwa kipindi cha miaka minne sasa tokea kuanza kupanda mbegu zilizofanyiwa utafiti, uwezo wake wa kuzalisha umeongezeka.

Alisema jambo jengine lililomvutia katika mbegu hizo ni jinsi zinavyostawi na kukabiliana na ukame pamoja na wadudu waharibifu.

Alisema kwa mbegu za zamani aina ya mwari, sepide na rikunde uzalishaji haukuwa mzuri na zilimrejesha katika umasikini.

Hata hivyo, alisema kwa sasa tatizo la chakula katika familia yake limeondoka kwa sababu muhogo na viazi vitamu anavyo kwa wingi.

“Mbegu hii ya kizimbani kwa sasa inanipa faida kubwa kwa familia yangu kuliko zile nyengine za zamani, ilikuwa nashindwa hata kupata chakula kwa ajili ya familia,” alisema.

Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekuwa ikiuwanga mkono wakulima kwa kufadhili shughuli za utafiti wa mbegu ili kuongeza uzalishaji wenye tija.