NA FATMA KASSIM

WAUGUZI na Wakunga nchini, wametakiwa kubadilika katika utendaji wa kazi zao kwa kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika kufuata huduma za afya katika hospitali na vituo vya afya.

Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga alieleza hayo katika mkutano wa kuimarisha utendaji kazi kwa viongozi wa wauguzi na wakunga wa hospitali ya Mnazimmoja na Al-Rahma.

Alisema katika kuimarisha utendaji wa kazi ni vyema wauguzi wakaleta mabadiliko ya utoaji wa huduma katika hospitali za serikali na binafsi kwa suala zima la kufuata maadili ya kazi zao na kuondosha malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wanaokwenda kufuata huduma.

Alifahamisha kuwa baraza la wauguzi na wakunga halitosita kumchukulia hatua muuguzi yoyote na mkunga ambae atakikuka maadili ya uuguzi na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

Alisema jamii pamoja na dunia kwa ujumla inatambua juhudi kubwa za utendaji wa kazi wanazozifanya, hivyo aliwataka kufanyakazi kwa bidii na kuepuka malalamiko kwa wananchi wanaokwenda kufuata huduma.

Kwa upande wake mrajis wa Baraza la Wauguzi na Wakunga, Vuai Kombo Haji aliwataka wauguzi na wakunga   wote nchini kufuata kanuni za maadili ya uuguzi na ukunga hali itakayoondosha malalamiko kwa wagonjwa.

Alisema uwajibikaji kwa wakunga na wauguzi una umuhimu mkubwa na wanapaswa kulinda utu wa mtu, kujali jinsia, kuwa na uadilifu, kuheshimiana, mawasiliano na ushirikiano, utaalamu pamoja na jitihada katika kufanya kazi kwa ufanisi.

Aliwasisitiza wajibu wa wauguzi kukata leseni zao za kazi kwani kufanya hivyo kutawawezesha kufanya kazi zao kwa uadilifu.

Nao baadhi ya wauguzi walisema kuwa katika kuleta mabadiliko katika kazi kunahitajika vifaa vinavyoendana na wakati ili kuwahudumia wagonjwa  kwa umakini.