NA KHAMISUU ABDALLAH

WALIMU wamesisitizwa kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanafunzi wao na badala yake kutimiza wajibu wao katika kuwajenga watoto kielimu.

Mbunge wa Viti Maalum, Wanu Hafidh Ameir,  aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanafunzi katika mahafali ya 15 ya kituo cha kujiendeleza Darajani Agreement Education Center yaliyofanyika katika ukumbi wa Baitul- Yamin Malindi.   

Alisema walimu wanaofanya vitendo hivyo wanachafua kada ya ualimu na kuondosha kiapo cha uaminifu wakati wakisomea kada hiyo ya kuwajenga wanafunzi kuwa viongozi bora wa baadae.

Aidha alisema ni ukweli usiopingika kuwa watoto wengi wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanakatishwa ndoto zao na malengo yao ya kuwa wataalamu bora wa taifa la Tanzania.

Mbunge Wanu, alibainisha kwamba ni jambo la kushangaza kuona walimu huwafanyia wanafunzi wao vitendo vya udhalilishaji hali inayorejesha nyuma juhudi za wanafunzi na serikali katika kupambana na vitendo hivyo.

“Nawapongezeni ni miaka 15, sasa nimekuwa mlezi wa kituo hichi sijasikia tukio lolote la udhalilishaji kwa wanafunzi endeleni kujiheshimu walimu wetu na kuifanya kazi hii ya wito kwa kuwajenga vijana watoto wetu kuona wanafanya vizuri katika mitihani yao ya taifa,” aliwashauri.

Hata hivyo, aliwasisitiza wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kulipa ada, ili kusaidia juhudi za walimu za kuhakikisha wanafanya vizuri katika mitihani yao ya taifa.

Aliupongeza uongozi wa kituo hicho kwa kuwandaa vijana katika kuona wanafanya vizuri, kwani hakuna kazi ngumu kama ya kulea watoto hao.

Hata hivyo, Mbunge Wanu, aliwasihi wanafunzi kujitahidi kusoma kwa bidii na kujiepusha na vitendo ambavyo zinaweza kuwaharibia maisha yao, ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa kwani elimu ni ufunguo wa maisha.

Wanu ambae ni mlezi wa kituo hicho aliahidi kuchukua jitihada za kushirikiana na Wizara ya Elimu, ili kituo hicho kiendelee kuwalea watoto kitaaluma.

Nae, Mtendaji Mkuu wa kituo hicho, Hafidh Rashid Abdullah, alisema lengo la kituo hicho ni kuendeleza masomo ya mchipuo wa biashara na lugha kwa mwaka 2021 kuona wanafunzi wanafanya vizuri na kukuza ushirikiano baina yao na tasisi mbalimbali.

Alisema kituo hicho, kimewekeza zaidi katika kuwasaidia vijana wa Zanzibar kuona wanapasi vizuri katika mitihani yao.

Nao wanafunzi wa kituo hicho walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vitabu vya sayansi na sanaa hali inayopelekea kutosoma ipasavyo.

Katika mahafali hayo wanafunzi mbalimbali walikabidhiwa zawadi ambapo mwanafunzi bora wa ujumla, alikuwa ni Riziki Ali Iddrisa,