KAMPALA,UGANDA

WANAHARAKATI wa haki za binadamu nchini Uganda wanatoa wito kwa serikali kumwachilia huru wakili wa haki za binadamu Nicholas Opio,ambaye alikamatwa kwa madai ya biashara ya kutakatisha fedha.

Wafuasi walisema Opio anatuhumiwa kwa uanaharakati wake.

Kikundi cha mawakili na wanaharakati walikwenda kwenye Kitengo Maalumu cha upelelezi cha polisi wa Uganda kudai kumwona Opio na kuwataka polisi wamwachilie huru.

Opio, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la haki za binadamu Chapter 4 nchini humo, alikamatwa Jumanne na wenzake wawili katika mgahawa mmoja jijini Kampala.

Kulingana na Chapter 4, Opio amekuwa akikusanya ushahidi kuhusiana na mauaji na ukamataji ambao ulitokea wakati wa siku mbili za maandamano nchini Uganda yaliyoanza Novemba 18.

Watu 56 waliuwawa katika mapigano kati ya wafuasi wa upinzani na vikosi vya usalama kufuatia kukamatwa kwa mwimbaji aliyeingia kwenye siasa Bobi Wine, kiongozi wa chama cha National Unity Platform.

Wakili wa haki za binadamu Elone Kiiza alisema Opio yupo kwenye ari nzuri,lakini haamini Opio ataachiliwa katika saa 48 za kawaida.