NA ZUHURA JUMA
WANANCHI kisiwani hapa wameshauriwa kuchangia damu, ili kuokoa maisha ya watu wengine wanaohitaji damu wakati wanapopatwa na tatizo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika bonanza
la uchangiaji damu
lililofanyika uwanja wa tenis Chake Chake, Ofisa uendeshaji tiba kutoka Wizara ya Afya Pemba, Dk. Yussuf Hamad Iddi
alisema, ipo haja kwa wananchi kuchangia damu
kwa ajili ya kuwasaidia
wennye matatizo.
Alisema wakati mwengine kunakua na upungufu wa
damu katika kitengo cha
damu salama, jambo ambalo linawapa wakati mgumu hasa anapotokezea mgonjwa ambae atahitaji damu kwa haraka.
“Damu ni kitu muhimu kuwepo katika kitengo
chetu, kwani wakati mwengine wanakuja
wagonjwa wa ajali ama akinamama wanaojifungua, hawa wakati mwengine wanakuwa na hali ya dharura hivyo
wanahitaji damu,” alisema.
Alisema bonanza hilo ni muendelezo wa mabonanza
mbali mbali wanayoyaweka kwa ajili ya
uchangiaji damu kwa, lengo la kuwasaidia watu
wenye matatizo.
“Tangu kipindi cha kampeni hatujaandaa bonanza
hili, hivyo tumekuwa na upungufu wa damu
na ndio maana tukaamua kufanya hivi,” alieleza.
Alisema katika bonanza hilo walitarajia
kukusanya
chupa (unit) 100 za damu lakini walipata chupa
20 tu kutokana na kuwa walengwa
hawakwenda kuchangia damu.
“Tulitarajia kupata watu wengi kwa vile siku
nyingi hatujafanya bonanza hili, ila wananchi hawakuitikia wito, ila tutafanya tena ili kuhakikisha tunapata damu ya kutosha”, alifahamisha.
Alieleza kuwa, wanachama wao wanapewa damu bure
wanapokwenda na wagonjwa
wao, lakini wasiokuwa wanachama wanalazimika kuchangia damu.
“Wanapokuja watu ambao sio wanachama, tunawatia
damu iliyopo lakini tunawambia lazima
walete mtu katika familia ili tupate damu, kwa sababu ile ni akiba na wala hawatoi fedha kwani damu ni haramu kuuzwa,” alisema.
Hivyo daktari huyo aliwaomba wananchi
wanaposikia mabonanza ya kuchangia damu
wajitokeze kuchangia.