NA MWANDISHI WETU PEMBA

WANANCHI kutoka vyama mbali mbali vya Siasa Kisiwani Pemba , wameipokea  hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk, Hussein Ali Mwinyi, alioitowa  Kisiwani Pemba wakati wa ziara yake ya mwanzo tokea kushinda uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka

2020-25 na kusema inaonesha mwanga wa matumaini. Wakizungumza na Gazeti hili wamesema hotuba hiyo  ilijaa kila aina ya dhamira za Dk, Mwinyi katika kuwaletea mema wananchi wa Zanzibar na hiyo imeonesha mwanzo mzuri wa uongozi wake kwa Zanzibar.

Walisema yote aliyoyaeleza ni ya halali na kwamba akitekeleza nchi ya Zanzibar itapiga hatuwa kubwa ya kimaendeleo hivyo wamewataka wananchi kumuunga mkono kwa dhamira zake hizo.

Wananchi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa walieleza kuwa inafaa Dk, Mwinyi kuchukuwa maamuzi magumu, ili kila mmoja aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo  ikiwemo kulinda mali za Serikali na utowaji wa huduma inavyostahiki.

Mwananchi Juma Ramadhan Ali  mkaazi wa Michakaeni, aliimbia Zanzibar Leo, hotuba ya Dk, Mwinyi, imejaa neema ila ameomba utekelezaji uwe wa vitendo, ili wananchi wazidi kuwa na imani na Serikali anayoiongoza.

“Mimi naamini kila alilolisema linaweza kufanikiwa iwapo kila mmoja atakuwa tayari kumpa mashirikiano ya kutosha nawaomba Viongozi waliomo kwenye Serikali ya awamu ya nane huu ndio wakati wa kuijenga Pemba, kwani wako makini ”alisema.

Akizungumzia suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wajuwe alilolifanya Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi ni jema na alilisimamia na kulitekeleza kwa matakwa ya kikatiba ya nchi.

Alieleza wale ambao hawajafahamu kuhusiana na hilo basi wasikilize kwenye vyombo vya habari au wakipata muda wasome katiba ya Zanzibar imefafanua hilo.

Bwana Rashid Ali Hamad, alisema amevutika na hotuba ya Dk, Mwinyi maana kwa mara ya mwanzo hajapata kusikia kauli  ya kiongozi mkuu wa nchi iliojaa maeneo yenye kusisimuwa kama aliotowa katika mkutano huo.

Akizungumzia suala la Rais wa Zanzibar Dk, Mwinyi , kutamka anania ya kuchukuwa maamuzi magumu juu ya wanaofuja mali za Umma alisema ni jambo la busara kwa wananchi wa Zanzibar kwani hilo limeonesha umakini wake juu ya kusimamia raslimali za nchi na kutaka kila mmoja heshimu mapato ya Serikali ili yawasaidie wananchi waliowengi .

“ Mimi nampongeza Rais wetu kwa azma yake ya kutaka kuchukuwa  maamuzi magumu na sisi tunaungana nae kwani kwa hali inavyokwenda Zanzibar yengefikia uchumi wa kati kuliko Tanzania bara,”alieleza.

Mussa Said Ali ,balozi wa nyumba kumi Jadida, alisema kauli ya Dk, Mwinyi, imewapa mwanga mkubwa na kujenga matumaini  ya maendeleo zaidi na alichokisema kina ashiria azma ya kweli alioitowa katika kipindi cha Kampeni ya Uchaguzi mkuu.

Alisema kila mwananchi na mpenda maendeleo wa nchi hii anapaswa kumuunga mkono Dk, Mwinyi kwa lile alilodhamiria kulifanya kwa Zanzibar, kwani ni kweli yajayo nineema na hili alilodhamiria ya kuchukuwa maamuzi magumu litakuwa jambo la heri kubwa kwa nchi hii.