NA MZEE GEORGE

KUTOKANA na kuongezeka kwa kesi ugonjwa wa malaria nchini, masheha, maofisa wa afya wa mabaraza ya manispaa na viongozi wa wilaya wa mkoa Mjini Magharibi, wamehimizwa kuwaelimisha wananchi kutoa mashirikiano wakati wa zoezi la upigaji dawa ya mbu majumbani litakapofanyika mwezi Februari mwakani.

Meneja wa programu ya kumaliza malaria Zanzibar, Abdalla Suleiman Ali alitoa wito huo katika mkutano wa uhamasishaji na utoaji taarifa za upigaji dawa majumbani uliofanyika katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja.

Alisema maradhi ya malaria bado yapo na yanaonekana kuongezeka hapa Zanzibar kutokana na wagonjwa kuripotiwa katika vituo mbali mbali vya afya na hospitali za Unguja na Pemba.

“Kesi nyingi za maradhi ya malaria zinaonekana kujitokeza katika vituo na hospitali zetu hapa nchini, licha ya jitihada kubwa za serikali kapambana na maradhi haya kwa kusema hivyo basi malaria ipo tujitahidi kujikinga nayo”, alisema Abdalla.

Aidha aliwataka wananchi kuendelea kutumia njia za kujinga na ugonjwa huo  ikiwemo kutumia vyandarua, kutumia tiba sahihi na kusafisha mazingira.

“Naomba sana wananchi wetu waendelee na utamaduni njia mbadala za kujikinga kwa kutumia vyandarua, lakini kuripoti mapema katika hospitali na vituo vya afya pale tu wanapohisi dalili ya homa za malaria ili wapatiwe matibabu ya haraka”, alisema.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa Mjini Magharibi katibu tawala wa mkoa huo Saleh Mohammed Juma, alisema viongozi wa mkoa, wilaya na manispaa watashiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kuhakikisha shehia zote zilizotakiwa kutiwa dawa zinafikiwa.

Hata hivyo, aliwaagiza viongozi wa wilaya zote za mkoa huo kuhakikisha hawawapangii kazi nyengine masheha wao siku ya zoezi la upigaji dawa litakapoanza katika shehia zao.

Wakitoa mada za uhamasishaji upigaji dawa na hali ya malaria, Makame Hassan Makame na Mwinyi Issa Khamis walisema zaidi ya wagonjwa 12,000 wameripotiwa kuwa na maradhi ya malaria katia vituo vya afya.

Walisema ili kufanikisha zoezi hilo lazima kutumike njia za kuwahamasisha wananchi kupitia vyombo vya habari, mikutano ya shehia pamoja na viongozi wa wilaya na shehia kuwa karibu wakati wa zoezi hilo.

Walisema zoezi hilo ambalo linatarajiwa kufanyika kuanzia Februari 19 hadi 23 mwakani zaidi ya watu 600 watapata ajira ya muda wakiwemo wapigaji dawa, madereva, mafundi na wahudumu.

Mapema wakizungumza kwa niaba ya masheha wenzao, masheha walioshiriki katika mkutano huo wameahidi kutoa mashirikiano ya kutosha na kuiomba wizara ya afya kitengo cha malaria kuwajulisha mapema siku iliyopangwa upigaji dawa kwa kila shehia ili nao waweze kuwaarifu mapema wananchi juu ya zoezi hilo.