NA MBARAKA KAMBONA, MANYARA
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amewataka wale wote wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu kuacha mara moja, kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa.
Gekul alitoa onyo hilo alipokuwa akiongea na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo Disemba 21, 2020.
Waziri Gekul, katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali, ili kukomesha vitendo hivyo.
“Hatutavumilia jambo hili liendelee, Sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema Gekul
Aliongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.
“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho ,” aliongeza Gekul.
Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia Vizimba na Mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu.
“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa Vijana, Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani, ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” alisisitiza Gekul.