NA ABOUD MAHMOUD
WATU wanne wamenusurika kufa baada ya jengo maarufu visiwani Zanzibar la Beit-al-Ajaib kuanguka likiwa linaendelea kufanyiwa ukarabati.
Majeruhi hao ni miongoni mwa mafundi wanaoendelea kulifanyia matengenezo jengo hilo, ambapo baada ya kuokolewa waliwahishwa hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya matibabu.
Majeruhi watatu kati ya wanne waliobainika majina yao ni Hamad Mattar Abdullah (39), Dhamir Salum Dhamir (37) wote wakaazi wa Kinuni wilaya ya Magharibi ‘A’ na Haji Chum Machano (37) mkaazi wa Chumbuni, ambapo mmoja ameokolewa lakini hakutambuliwa jina lake.
Mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo baadhi ya viongozi wakuu wa serikali walifika katika eneo hilo akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza baada ya kupewa maelezo, Dk. Mwinyi alisema mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uokoaji utafanyika uchunguzi wa kina kujua nini chanzo cha kutokea kwa ajali hiyo.
“Jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu waliokwama, lakini mara baada ya kumalizika kwa kazi ya uokozi na kupatikana wote tutashughulika na mambo mengine ikiwemo uchunguzi wa tukio hili”, alisema Dk. Mwinyi.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alizitaka taasisi mbali mbali za uokozi kushirikiana katika kuhakikisha watu wote waliokwama wanapatikana.
Aidha Makamu alisema serikali ipo tayari kushirikiana nao katika kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi na kuokoa maisha ya waliokuwemo ndani ya jengo hilo.