KINSHASA,DRC

RAIA wasiopungua 34 wameuawa katika kipindi cha wiki mbili, baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha katika jimbo la Kivu Kaskazini na Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya watalaamu wa masuala ya usalama kutoka Security Barometer of Kivu (KST).

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, watu hao waliuawa kati ya Novemba 29 hadi Desemba 12 mwaka huu, huku wengine 19 wakitekwa na watatu wakijeruhiwa katika majimbo mawili.

Kati ya visa vitatu vilivyoripotiwa na watalaamu hao, vitatu vilitokea katika Wilaya ya Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini huku watu 25 wakiuawa baada ya kushambuliwa na kundi la waasi la ADF.

Huko Rutshuru, watu wasiofahamika, waliwateka nyara wanaume wawili na wasichana watatu, na kutaka kikombozi cha Dola Elfu tano ili kuwaachia huru.

Kundi la ADF linaendelea kuwa hatari sana katika majimbo hayo mawili na linatuhumiwa kutekeleza mauaji ya zaidi ya watu mia nane, kila mwaka.

Kundi la waasi kutoka Uganda la Allied Democratic Forces (ADF) limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Congo DR tangu muongo wa 90.

Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa uwanja wa mapigano na mauaji kwa miaka 20 sasa. 

Kushindwa jeshi la serikali na askari wa kofia buluu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kukabiliana vilivyo na waasi ni moja ya sababu kuu za kukosekana utulivu na amani katika maeneo hayo.