NA ABOUD MAHMOUD

WANANCHI wa visiwa vya Zanzibar wameshauriwa kusahau yaliopita na kuungana kwa pamoja kujenga nchi kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Makamo Mweyekiti wa Taasisi ya G1 Mapinduzi Kwanza,Ramadhan Ali Kimara wakati alipokua akizungumza na Zanzibar Leo ambapo alisema kuundwa kwa Serikali ya Umoja Kitaifa ni kwa ajili ya kuwaletea mafanikio wananchi wake.

Makamo huyo alisema huu si wakati wa wananchi kukumbuka ya nyuma ambayo yatasababisha kuendeleza chuki na hasama bali ni kuendeleza mashirikiano ambayo yataweza kuwapa nguvu viongozi kufanya mabadiliko kwa pamoja.

“Nawaomba wananchi wezangu tusahau yaliopita sisi ni wamoja ni vyema kusahau ya nyuma na tushirikiane kwa pamoja sisi na viongozi wetu kwa ajili ya kuleta maendeleo ya haraka hapa nchini kwetu,”alisema.

Kimara alisema kwamba kuwepo kwa umoja katika nchi ni jambo jema kwani hata dini zinahamasisha waumini wake kuwa kitu kimoja na kuondosha tofauti walizonazo ambazo zitasababisha kufarakana.

Alisema kwamba wananchi wanatakiwa kutambua kwamba siasa ina muda wake na baada ya kumalizika watu wote wanatakiwa kushirikiana katika shughuli mbali mbali za kijamii.

“Siasa ni sawa na mpira wakati wakiwa uwanjani wanagombana lakini wakimaliza wanakua kitu kimoja hivyo na sisi wanasiasa tuwe hivyo hivyo tukimaliza mambo hayo tushirikiane katika mambo mbali mbali na sio kuhasimiana tukifanya hayo nchi yetu hatutoijenga,”alisema.

Makamo Mwenyekiti huyo alisema G1 Mapinduzi Kwanza inampongeza Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi na Makamo wa Kwanza Maalim Seif Shariff kushirikiana kwa pamoja kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kueka pembeni siasa.

Alisema G1 inaamini mashirikiano hayo baina ya viongozi hao wawili yatasaidia kuiletea maendeleo ya haraka Zanzibar katika kipindi kifupi cha uongozi wao  wa pamoja.

“Nawapongeza viongozi nwetu hawa wawili kwa kukubali kwa ridhaa yao kuunda serikali ya umoja wa kitaifa naamini lengo lao ni kuiokoa nchi yetu isifike katika hatua mbaya na mashirikiano yao wamejua kwamba yatasaidia kuteta maslahi ya Wazanzibari wote,”alifafanua.

Aidha Kimara alimuomba Makamo wa kwanza kutumia njia kama anazozitumia Dk Mwinyi kuhamasisha wananchi kuondosha chuki, hasama na kushirikiana katika kuijenga Zanzibar.

Alisema wananchi wa Zanzibar wamekua wakizifurahia hotuba mbali mbali zinazotolewa na Dk Mwinyi katika maeneo mbali mbali ambazo zinahamasisha kuondosha tofauti walizonazo na kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo .