NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji na Maliasili ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la Paje, Dk. Soud Nahoda ameahidi kutoa shilingi milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kuchangia malipo ya mishahara kwa walimu wa maandalizi wa skuli ya Jambiani Kibigija Mkoa wa Kusini Unguja.

Hatua hiyo imekuja baada ya waziri huyo kupokea changamoto juu ya ukosefu wa mishahara kwa walimu wa skuli hiyo inayoendeshwa na jamii katika hafla fupi ya mahafali iliyofanyika Jambiani Kibigija.

Alisema serikali ya awamu ya nane imedhamiria kuimarisha ufanisi wa sekta mbali mbali ikiwemo elimu ili watoto wajengwe katika misingi bora na imara itakayosaidia kuchangia mabadiliko ya maendeleo nchini.

Aidha alisema ili kufikia lengo hilo lazima kuwe na mipango, mikakati endelevu itakayosaidia kutoa matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kuwaondolea changamoto walimu ambazo zinazowakabili ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

Waziri huyo, aliahidi kuwa mstari wa mbele katika kuondosha matatizo yanayowakabili walimu na wanafunzi jimboni humo ili watoto wasome kwa ushindani, ari na bidii pamoja na kutimiza ndoto zao za mafanikio ya elimu.

“Na ili wazee wenzangu tuweze kuleta mabadiliko ya elimu jimboni kwetu lazima tushirikiane kwa pamoja katika kufuatilia mwenendo na tabia za watoto wetu ili kuona wanafuata maadili, silka na utamaduni Wazanzibari ambao ndio njia pekee inatakayosaidia kutimiza utu wao”, alisema.

Alisema serikali ya awamu ya nane ni yenye kutaka maendeleo na kusimamia malengo ya mapinduzi ya mwaka 1964 ikiwa ni pamoja na kuondosha matabaka ubinafsi katika suala zima la elimu.

Alifahamisha kwamba mkazo wa serikali umewekwa katika uandikishaji wa watoto na kuimarisha ubora wa elimu na mazingira bora ya ufundishaji na ujenzi wa skuli za kisasa.

Wakati huo huo Waziri huyo wakati akiweka jiwe la msingi katika skuli ya maandalizi na msingi ya New Golden Academy katika shamrashamra za mahafali ya pili huku Kizimbani alikabidhi shilingi milioni moja kwa ajili ya muendelezo wa ujenzi wa skuli hiyo.

Alisema lengo ni kuona Zanzibar inapiga hatua katika ushindani wa elimu bora ili watoto wasome vizuri na kuleta ufaulu bora.