NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amewataka viongozi wa klabu za michezo kuwa wabunifu na kushirikiana na wadau kujenga ofisi zitakazowasaidia kuendesha shughuli zao.

Alitoa wito huo wakati wa ufunguzi wa ofisi ya klabu ya soka ya Jang’ombe Boys na kueleza hatua hiyo ni ya kupongezwa na ni ya mfano kwa klabu nyengine kufata.

Alisema kuwa hatua ya klabu kuwa na ofisi ni nzuri na itasaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Hivyo alisema kuwa uamuzi wa klabu hiyo katika kutafuta ofisi ni mzuri sana na kuwataka waitumie ofisi hiyo kwa malengo ambayo yamekusudiwa ili kuimarisha viwango vya wachezaji wao.

“Naamini hii ni sehemu nzuri ambayo kila mmoja wenu ameiona na lengo kubwa la kuwa na ofisi hii ninavyohisi si jengine bali ni kuweza kufanya majukumu yenu kwa ufanisi ili kuendeleza vipaji vya vijana,” alisema Tabia.

Hivyo aliwataka viongozi wa klabu hiyo kuhakikisha wanafanya yale ambayo wamejipangia katika mipango yao ya kila siku ili kuhakikisha klabu yao inazidi kuwa juu kimaendeleo.

Mapema Katibu wa klabu hiyo Alawi Haidar Foum, alisema kuwa jengo la ofisi yao limepatikana kwa jitihada kubwa za viongozi wa klabu hiyo pamoja na viongozi wa jimbo lao akiwemo Mbunge na Mwakilishi ambao kwa kiasi kikubwa wamewasaidia mpaka kufikia hapo.

Jang’ombe Boys katika msimu wa 2020/2021, inatarajiwa kushiriki ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja baada ya msimu uiopita kushuka daraja kutoka ligi kuu.