NASRA MANZI NA RAYA HAMAD

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amezuia makubaliano yote yanayoihusisha Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu.

Waziri huyo alitoa agizo hilo kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu na waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohammed Mussa.

Haroun alisema kwa sasa makubaliano yote yanayohusu mikataba na taasisi hiyo yamesimamishwa ili kuipa nafasi serikali kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika hadi kufikiwa kwa makubaliano.

Alisema serikali kupitia taasisi hiyo ina nia njema ya kuwa na mashirikiano lakini isiwe makubaliano ya kunufaisha upande mmoja ila yawe yanazinufaisha pande zote.

“Kuna nyaraka zilizowahi kuibiwa na waliotoa ni wafanyakazi kutoka taasisi hii serikali ikachukuwa hatua kwa wale waliohusika, lakini inasikitishwa sana kuona kumbe maradhi haya hayajesha”, alisema.

Aidha waziri Haroun alikemea tabia na mtindo uliozuka hivi sasa kwa baadhi ya wafanyakazi na watendaji wa serikali wasio waaminifu kutoa siri za serikali na kuzisambaza kupitia magurupu mbalimbali ya mitandao ya kijamii jambo ambalo ni kinyume na maadili na taratibu za kiutumishi 

“Kuanzia sasa mfanyakazi yeyote wa serikali tukimbaini na akijulikana anatoa siri za serikali hatua kali za kisheria zitachukuliwa, naomba wafanyakazi na watendaji waelewe kuwa tunafuatilia kwa makini wale wanaovujisha siri za serikali na baadhi yao tayari tumeshawapata na watachukuliwa hatua za kinidhamu”, alisema.

Kwa upande wake, waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohammed Mussa alisema nyaraka ni rasilimali muhimu zinazohitaji kuangaliwa kwa umakini, hivyo alimuomba waziri Haroun kuhakikisha anachukua mikakati ya kuzilinda nyaraka.

Aidha Lela alimuomba waziri Haroun kuangalia makubaliano yaliyofikiwa kati ya taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Zanzibar na taasisi nyengine kama makubaliano hayo yana maslahi.

Lela alikabidhi taarifa ya utendaji kwa kipindi cha miaka mitano, muundo wa taasisi  na vitengo mbalimbali, nakala za baadhi ya nyaraka zilizowahi kuibiwa na kupatikana na nyaraka za makubaliano yaliyofikiwa na taasisi hiyo.