NA MWAJUMA JUMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imetoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara ambao wameficha mafuta ya kupikia kuyatoa katika maghala na kuyauza kwa wananchi kwa bei kawaida badala ya kuyapandisha bei.

Agizo hilo, limetolewa na Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, Mudrik Ramadhan Soraga, alipozungumza na waandishi wa habari huko Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kufatia kuongezeka kwa bei ya mafuta ya kupia ya OKI ambayo sasa hivi yanauzwa dumu moja la lita 20 kwa shilingi 58,000 kutoka 48,000.

Alieleza kuwa kumekuwepo na wafanyabiashara wakiwa wanategea kwa makusudi na kuyaficha mafuta hayo, ili wakiona yametetereka wanayatowa na kuyauza kwa bei ya juu, hivyo kwa upande wao watahakikisha kwamba akiba ambayo wanayo inatoka na kuingia sokoni.

Hivyo, alisema kuwa iwapo agizo hilo halitotekelezwa Serikali itakuja na kutoa bei elekezi.

Alisema kuwa awali kulijitokeza changamoto ya kupanda maradufu kwa mafuta hayo, lakini sasa hivi mafuta hayo yapo ya kutosha na kuwataka wananchi wasiwe na wasiwa na bidhaa hiyo.

“Tamko la wizara kwamba wafanyabiashara ambayo mafuta wanayo na kama walinunuwa kwa bei ya zamani wasiyauze kwa bei ambayo ipo sasa hivi”, alisema.

 “Hivi karibuni tulipokea changamoto ya soko la mafuta ya kupikia kutoka kwa wananchi na kwa baadhi ya vyombo vya habari kwamba bei ya mafuta hayo imeongezeka mara dufu, ambapo mafuta hayo yalipanda kutoka shilingi 48,000 hadi 58,000”, alisema.

Alisema kuwa kimsingi hali ya soko la mafuta kwa Zanzibar sasa hivi lipo vizuri, na wana tani zaidi ya 2,430 na wastani wao wa matumizi kwa mwezi ni tani 418 , hivyo wana akiba ya zaidi ya miezi sita ya mafuta ambayo yapo ndani ya soko lao.

Hata hivyo alisema sababu kubwa ambayo ilipelekea mafuta hayo kuongezeka kwa bei ni kutokana na kupanda kwa bei hiyo ya mafuta katika soko la dunia ambapo mafuta ya dumu la lita 20 linauzwa kati ya dola 20 mpaka 25 na uingizaji wa ndani ni shilingi 55,000 mpaka 58,0000.

Aliitaja sababu nyengine ya kuongezeka kwa bei ni kuongezeka kwa bei  ya soko la dunia ambayo nayo imebadilika, lakini vile vile kuna mahitaji makubwa ya mafuta nchini China ambao wanahitaji tani milioni 1.7 mpaka kufikia mwaka 2023, na hali iliyopelekea meli nyingi kusafirisha mafuta huko badala ya kuja huku.

Hata hivyo alisema kuwa yapo matarajio makubwa sana ya kupunguwa kwa mafuta katika kipindi cha miezi michache ijayo, huku Idara ya Biashara ikifatilia kwa karibu taarifa ya ziada ili iweze kuingia katika mfumo sahihi na kupata bei zinazostahili.

Sambamba na hayo, alisema kuwa bado wana kazi kubwa ambayo itabidi waifanye ya kupata taarifa za uhakika zaidi kabla ya kutoa bei elekezi.

Alisema wakishajiridhisha kwamba kuna tatizo hilo na kwa sababu wanayo mafuta ya kutosha na ikionekana kuna tatizo la bei linaenda zaidi ya ambavyo haziendani hatua ya bei elekezi itachukuliwa.

“Sasa hivi ni mapema sana kusema hivyo mpaka pale ambapo tutajiridhisha ndio tutatoa bei elekezi”, alisema.

Hata hivyo, uchunguzi wa Zanzibar Leo ulibaini kwamba bei ya mafuta kwa lita 20 yanauzwa kati ya shilingi 62,000 na 61,000, lita 10 yanauzwa kati ya shilingi 32,000 na 31,000 na lita tano yanauzwa shilingi 16,000 kwa baadhi ya maduka ambayo yapo katika soko la Mwanakwerekwe.