NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amewasimamisha kazi wakurugenzi wa mabaraza ya Manispaa ya Mjini na Magharibi ‘A’, kupisha uchunguzi zaidi juu ya upotevu wa fedha.

Waliosimamishwa ni mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Said Juma Ahmada na Amour Ali Mussa mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Vuga, alisema uamuzi huo umekuja kufuatia ripoti zilizowasilishwa kwake na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) na kupitia vyanzo vyengine kuonesha kuwepo dalili za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema katika uchunguzi huo imebainika kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha na kuamua kuchukua maamuzi hayo ambayo yana lengo la kuondosha shaka dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi, ubadhirifu, urasimu, muhali na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Aidha alimuagiza mkurugenzi atakaekaimu katika Manispaa ya Mjini kuupitia upya mkataba kati ya manispaa hiyo na kampuni ya ECONEX inayofanya kazi ya kukusanya mapato ya maegesho.

Alisema mkataba huo unaonesha mapungufu mengi na kumtaka kufanya hivyo ndani ya wiki mbili zijazo na kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba huo na sio vyenginevyo.

Kutokana na kadhia hiyo waziri Masoud, aliwaagiza wakurugenzi wa mabaraza ya manispaa, mabaraza ya miji na halmashauri za wilaya kubadilisha watendaji wote wanaohudumu katika vitengo vya fedha, manunuzi na mapato.

Aidha aliwaagiza wakurugenzi hao kusimamia kikamilifu suala la ukusanyaji wa kodi na tozo zilizopo katika vyanzo vya mapato vilivyomo katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyengine waziri huyo amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), kuivunja bodi ya zabuni ya jeshi hilo kupisha uchunguzi zaidi na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa kuunda bodi mpya.

“Mkuu nakuagiza kuwaweka pembeni watendaji wa kitengo cha hesabu, kitengo cha manunuzi, kitengo cha mipango na kitengo cha usimamizi wa miradi na kupisha uchunguzi zaidi kufanyakazi yake,” alisema.

Aidha waziri huyo aliwaagiza wakuu wa Idara Maalum za SMZ kufanya uhakiki wa watumishi wote kwa mwezi wa Januari 2021 ili mishahara yote ilipwe kupitia dirishani badala ya benki ili kukidhi matakwa ya uhakiki huo ili kujiridhisha kuwa hakuna wafanyakazi hewa.

Akizungumzia utendaji wa masheha, Waziri huyo aliwaagiza wakuu wa mikoa kutathmini upya uwezo na utendaji kazi wa masheha wote na kamati zao za shehia, endapo watabaini kuna udhaifu watengue uteuzi wao.

Kuhusu kituo cha afya, waziri Masoud alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, kuhakikisha nyumba ya kituo cha afya Uroa iliyobomolewa na mtu aliyepatiwa nyumba hiyo kinyume na utaratibu ahakikishe kuwa wote waliohusika wanafikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.