NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mambo ya Nje Jamhuri ya China, Wang Yi, anatarajia kufanya ziara ya siku mbili kuanzia Januari saba hadi nane 2021, huko Chato Mkoani Geita nchini Tanzania .
Akitoa taarifa hiyo mbele ya wandishi wa habari jijini hapa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema ziara hiyo inalengo la kuimarisha uhusiano na mashirikiano ya kiurafiki na kiujamaa kwa nchi ya Tanzania na China.
Alisema katika ziara hiyo watajadili masuala mbali mbali ikiwemo miradi, ili kuhakikisha nchi zinaendelea vizuri na zinasaidia katika kuleta maendeleo baina yao .
Prof. Kabudi alisema uhusiano huo ni wa kihistoria ambao umetimiza miaka 55, tangu kutiliana saini mkataba wa urafiki uliosainiwa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Hayati Mwalim Julius Nyerere alipotembelea China kwa mualiko aliopewa na mkombozi wan chi hiyo.
Alisema ziara hiyo ni muhimu na imekuja mara baada ya mazungumzo ya simu yaliyofanyika mwezi huu (Disemba), kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Watu China Xi Jinping.
Aidha alieleza katika mazungumzo hayo wamejadili mambo mengi ikiwemo uhusiano wa kirafiki na biashara kwa nchi mbili hizo.
Aliongeza maeneo mengine ambayo nchi hizo mbili zinasimama pamoja ni katika siasa za Kimataifa ikiwa pamoja na mabadiliko ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Alieleza mbali ya kuwa na changamoto ya Ugonjwa wa Covid 19 bado kwa upande wa biashara kati ya Tanzania na China kumekuwa na mafanikio makubwa, ambapo katika mwezi huu, ulifanyika mkutano kwa njia ya mtandao kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania na Kampuni ya Albaba ya China.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuziwezesha kampuni za Tanzania kuuza bidhaa China, Tanzania kwasasa imekubaliwa kuuza maharage ya soya katika nchi hiyo ambayo yanasoko kubwa kwa sasa.