HARARE, ZIMBABWE

SHIRIKA la mpango wa chakula Duniani (WFP) limetoa wito kutolewa fedha za dharura katika kipindi cha miezi sita ijayo, ili kuwasaidia raia milioni nne wa Zimbabwe wanaokabiliwa na baa la njaa.

Mgogoro wa kiuchumi ambao nchi hiyo ulipitia kwa miaka 20 iliyopita umezidi kuwa mbaya pamoja na janga la COVID-19 na raia kwa sasa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambalo ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Tuzo ya Nobel limeeleza kuwa, linahitaji kukusanya zaidi ya dola milioni 200, au karibu euro milioni 160, kwa msaada wa chakula wa haraka nchini Zimbabwe, hasa katika maeneo ya vijijini.

Miaka kadhaa mfululizo ya ukame tayari ilidhoofisha usalama wa chakula nchini Zimbabwe na mavuno ya mwaka huu yameathiriwa tena.

Kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Fedha ya Zimbawe, uagizaji wa chakula katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu umeongezeka mara tatu ikilinganishwa na mwaka jana.

Wakati huo huo janga la Corona limedhoofisha uchumi ambao tayari unalegalega, na mfumko wa bei ambao unasababisha bei za bidhaa mahitajio kupanda mara dufu.

Hivi karibuni pia, mashirika ya Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) yalitahadharisha kuhusu njaa katika maeneo kadhaa duniani.

Ripoti ya FAO ilisema mamilioni ya watu katika nchi nne zilizoghubikwa na tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula za Burkina Faso, Kaskazini mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen wanahitaji msaada wa chakula ili kuepuka kutumbukia katika baa kubwa la njaa.