NA HAFSA GOLO

WIZARA ya Kilimo, Umwagiliaji na Maliasili imesema itahakikisha inashirikiana bega kwa bega na Halmashauri ili ujenzi wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji unatimiza malengo yaliokusudiwa na serikali.

Waziri wa wizara hiyo Dk. Soud Nahoda, alieleza hayo wakati akizungumza na wakulima wa zao la mpunga, timu ya wataalamu na watendaji katika bonde la mpunga Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema atahakikisha miundombinu inayojengwa katika maeneo mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba inafuata masharti na vigezo vya kitaalamu ili mradi huo uwe wenye manufaa kwa wakulima na serikali kwa jumla.  

Dk. Soud aliwataka wataalamu wazalendo wanaousimamia mradi wa Ujenzi wa Umwagiliaji Maji nchini kufuata maelekezo ya mikataba, sheria na miongozo kwa dhamira moja ya kuondosha vikwazo vitakavyochangia kuleta changamoto ya utekelezaji wake.

“Nakuombeni muongeze ari na bidii katika usimamizi wa mradi huo ili azma ya serikali na malengo ya wakulima yatimie kwa wakati,” alisema Nahoda.

Aidha alisema, katika hekta 184 zilizopo kwenye bonde la Kinyasini, wakulima 526 wakiwemo wanawake 300 watafaidika na mradi huo utakapokamilika.

Alifahamisha kwamba, serikali kupitia mradi huo imedhamiria kuwaondolea wakulima wa zao la mpunga changamoto zinazowakabili kwa kuongeza uzalishaji utakaopunguza umasikini wa kipato na chakula.

“Katika hekta 184 ambazo zinatarajiwa kulimwa kilimo cha biashara na wakulima hao tunatarajia ndani ya miezi mitatu zitavunwa tani 1,500,” alisema. 

Katika hatua nyengine waziri huyo, alisema kabla ya kuanza utekelezaji wake mradi huo aliagiza kupatiwa elimu wakulima hao kwani kufanya hivyo itasaidia kusimamia majukumu yao kwa ufanisi sambamba na kutumia njia za kitaalamu zinazohitajika.

Kuhusu pembejeo na mbolea aliahidi kwamba wakulima hao watapatiwa kwa muda unaostahiki huku akihakikisha mabibi na mabwana shamba wanatimiza wajibu wao.

Hata hivyo, waziri huyo, alisifu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na wataalamu wazalendo kwa kushirikiana na watendaji katika usimamizi wa mradi huo huku akihimiza uadilifu na uchapakazi uliobora zaidi.

Nao wataalamu hao waliahidi kusimamia vyema mradi huo ambao una maslahi mapana kwa wakulima na taifa kwa jumla.