NA AMEIR KHALID
CHAMA cha Mpira wa Mikono (Handball) Zanzibar ZAHA, kimeelezea masikitiko yake makubwa kwa timu za Zanzibar kushindwa kuthibitisha kushiriki mashindano ya kombe la Mapinduzi pamoja na mafunzo ya waamuzi.


Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza kesho Disemba 29, ambapo hadi tunakwenda mitamboni walimu 25 wamejitokeza kuomba mafunzo hayo ya uamuzi.


Akizungumza na gazeti hili Katibu wa chama hicho Zanzibar Mussa Abdul- rabi Fadhili, alisema mafunzo walitarajia zaidi ya watu 50 kushiriki lakini muamko umekuwa mdogo.


Alisema mafunzo hayo ni muhimu kwani hivi sasa sheria za mchezo huo nyingi zimebadilika, hivyo zingewasaidia kujua sheria mpya ambazo zinatumiwa na mashirikisho ya mchezo huo duniani kote.


‘’Sijui tunaelekea wapi, tunapotoka nje tunaposhindwa tunalaumu waamuzi kumbe tunazo sheria za zamani ,kujifunza tumekuwa wagumu sana.Pia tunalalamika mashindano, leo yapo kwetu tunashindwa kuthibitisha tuliowaalika wamezongwa na covid tu ndio hawakuweza kutoka kwao’’alisema.


Kuhusu mashindano ya kombe la Mapinduzi ambayo yalipangwa kufanyika hapa Zanzibar, Mussa alisema yataanza Januari 3 ambapo timu kutoka nje ya Tanzania hazitashiriki mwaka huu kutokana na janga la virusi vya corona, licha ya awali kuonyesha nia njema ya kutaka kushiriki.


Alitaja timu za hapa Tanzania ambazo zitashiriki ni Nyuki, JKU na JKT kwa wanaume na wanawake ni JKU na JKT.


Hata hivyo Mussa alielezea masikitiko yake makubwa kwa timu za Zanzibar kushindwa kuthibitisha licha ya kupewa barua tangu Oktoba 16 na tarehe ya mwisho wa kuthibitisha ni Januari 1, 2021.


Kwa upande wa timu za vijana alisema matarajio yao zitashiriki timu za Victori na Mlamleni kutoka Tanzaina bara na Mwanakwerekwe ya Zanzibar zote wanaume.


Kuhusu timu za Pemba Mussa alisema hapo awali walitarajia kuleta timu tatu, mbili za wanaume na moja ya wanawake, lakini hadi sasa hakuna uhakika wa kupata timu hizo.