NA ZAINAB ATUPAE
TIMU ya soka ya Jumuiya ya Zanvarsity Alumni imeshindwa kutambiana baada ya kutoka na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sulubu ya Pwani Mchangani ikiwa ni mechezo wa kirafiki.


Mchezo huo uliopigwa uwanja Pwani Mchangani majira ya saa 10:00 jioni.


Sulubu ndio iliokuwa ya kwanza kuwasubu wapinzani wao kwa kuziteketeza vyavu za Alumni kwa kufunga bao la kwanza lililofungwa na Yussuf Othman dakika ya 12 ,huku bao la kusawazisha la timu ya Jumuiya ya Zanvarsity likiwekwa wavuni na Mustafa Abdulhamid dakika ya 34 kwa njia ya penalti.


Mabao hayo yalidumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza ambapo timu zilitoka nje kwa ajili ya kupata mapumziko mafupi.


Kurudi tena uwanjani kumalizia kipindi cha pili timu hizo ziliingia kwa kasi kubwa,huku kila mmoja akifanya mabadiliko.


Mabadiliko yalianza kuleta mafanikio kwa timu ya Sulubu katika dakika ya 56 Said Dude kuongeza bao la pili,huku bao la kusawazisha la timu ya Alumni lilifungwa na Nasri Mhamed ‘Jeba’ dakika ya 78.