NA LAILA BAKAR

IDARA ya Makumbusho na Mambo ya Kale Zanzibar imesema inampango wa kujenga makumbusho kubwa ya kitaifa visiwani hapa.

Imesema makumbusho hiyo itaweza kubeba  kumbukumbu za aina tofauti ndani yake na kuweza kuingia katika haiba ya makumbusho za dunia.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Division ya Mambo ya Kale, Abdalla Khamis Ali, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii kwenye ukumbi wa Idara hiyo Nyumba ya Watoto Forodhani.

Alisema moja kati ya soko la utalii visiwani hapa ni makumbusho ambayo yamebeba  historia na urithi wa mambo ya kale, hivyo kuwepo kwa makumbusho ya kitaifa kutaifanya Idara hiyo kukusanya kiwango kikubwa  cha fedha ukilinganisha na makusanyo yaliopo sasa kutokana na ongezeko la watalii linavyokuwa kila mwaka.

Alisema visiwa vya Zanzibar vinatambulika zaidi katika soko la utalii mbali na makumbusho ya kitaifa ya Beit-al Ajab, inayojulikana kwa jina la (house of wonder) ambayo inafanyiwa ukarabati na ilikuwa ikiingiza fedha nyingi kutokana na mvuto wa jengo na historia yake.

Hata hivyo, alifahamisha kwamba mbali ya makumbusho hiyo ni vyema kuwa na makumbusho kubwa zaidi itakayobeba kumbukumbu aina mbali mbali.

“Makumbusho hiyo itakayojengwa itaweza kubeba makumbusho mbalimbali ndani yake ikiwemo utamaduni wa mzanzibari, makumbusho ya michezo, makumbusho ya mpira, makumbusho za Rais wa Zanzibar na nyenginezo, jambo ambalo litaweza kuvutia watu wengi wa ndani na nje ya nchi kwani kutakuwa na muonekano tofauti,”alisema.

Alisema katika nchi zilizoendelea kama China, Itali, Ugiriki, French, Ufaransa kwenye urithi wa mambo ya kale unapewa thamani kubwa kwa kuhifadhiwa, kulindwa na kuenzi vitu vyote vya kale.

Aidha alisema wamekuwa wakifanya hivyo kwani ndivyo vilivyobeba makumbusho na historia nzima ya nchi na ndio vitu ambavyo huwashawishi na kuwavutia wageni kutembelea ili kujua historia za nchi mbalimbali.