NA SABIHA KHAMIS, MAELEZO  

MAKAMU Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Mabrouk Jabu Makame amesema asasi za kiraia ni wadau muhimu katika ukuzaji wa demokrasia nchini.

Makamu huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waangalizi wa ndani wa uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mwezi Oktoba na viongozi wa vyama vya siasa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa waangalizi hao katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo ofisi za ZURA Maisara.

Alisema waangalizi wa uchaguzi ni watu muhimu katika kufanikisha maendeleo ya uchaguzi wa demokrasia hasa ikizingatiwa kwamba taarifa za makundi ya waangalizi husaidia Tume kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi ili kuondoa mapungufu.

Aliwataka viongozi wa taasisi za waangalizi wa uchaguzi wa ndani kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ili iweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya kidemokrasia.

Aliwaeleza waangalizi wa uchaguzi wa ndani kwamba wapo wananchi wamepoteza vitambulisho vya kupigia kura na wanaotaka kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda jengine waliotimiza vigezo vya sheria hivyo wanahitaji kuelimishwa ili kupata haki yao hiyo ya msingi.

Aliwapongeza viongozi wa taasisi hiyo kwa kazi nzuri waliyofanya katika kipindi chote cha zoezi la uchaguzi mkuu wa 2020 na kuandaa taarifa ambayo imegusa maeneo yote ya Zanzibar.

Aliahidi kuifanyia kazi taarifa ya waangalizi wa uchaguzi wa ndani na kuyafanyia kazi mapendezo yaliyowasilishwa ili kufanya chaguzi bora za kitaifa, kikanda na Kimataifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Uangalizi wa Ndani wa Uchaguzi, Abdalla Maulid Diwani aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwapatia kibali cha uangalizi wa uchaguzi wa mwaka 2020.

Alishukuru kwa kupatiwa mafunzo ya sheria za uangalizi wa uchaguzi yaliyowasaidia kukamilisha zoezi hilo kwa umahiri na umakini wa hali ya juu.