NA MAULID YUSSUF, WEMA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kampuni ya ZECCON wametiliana saini hati maalum ya kukabidhiana jengo la Chuo cha Mafunzo ya Amali lililopo katika kijiji cha Daya baada ya kukamilika ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idrissa Muslim Hija alisema kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa chuo hicho ipo haja ya kuanza kutumika ili vijana waweze kunufaika kitaaluma.

Alieleza kuwa matarajio ni kuhakikisha chuo hicho kinaanza kutoa masomo kuanzia mwezi Februari mwakani ambapo utoaji wa mafunzo hayo utakwenda sambamba na chuo cha Amali kilichopo Makunduchi.

Dk. Idrissa aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali kuweka utaratibu maalumu na kuandaa mazingira kwa ajili ya wanafunzi watakaoanza kusoma katika chuo hicho.

Katibu huyo aliishukuru kampuni ya ZECCON kutoka Tanzania bara kwa kukamilisha kazi hiyo kwa kiwango kinachoridhisha na kuwapongeza wote walioshiriki kwa namna moja ama nyengine katika kuusimamia ujenzi huo tokea ulivyoanza hadi kukabidhiwa.

Kwa upande wake mkandarasi wa ujenzi wa Chuo cha Amali Daya, Ali Mbarouk Juma aliishukuru wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kumuamini na kumpatia kazi hiyo ambayo tayari imekamilika katika kiwango kilichotakiwa.

Pia alieleza kuwa atayafanyia kazi yale yote ambayo wizara imemuomba kuyakamilisha na kuahidi kuyakamilisha bila ya malipo yoyote, ikiwemo ufungaji vipoza hewa (AC) katika chumba maalum cha kompyuta.

Naye mshauri elekezi wa mradi huo Mohammed Suleiman Nassor aliipongeza wizara ya Elimu kwa mashirikiano makubwa waliyowapatia kwa kipindi chote cha ujenzi wa chuo hicho ambapo wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wao kadri watakapohitajika.

Makabidhiano hayo yamefanyika baina ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kampuni ya ZECCON kutoka Tanzania Bara kwa kushirikiana na mshauri elekezi wa Mradi huo.