NA MWAJUMA JUMA
TIMU ya soka ya Shirika la Umeme (ZECO) inaondoka leo Disemba 24, kuelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya ziara ya kimichezo.
Timu hiyo inatarajiwa kuondoka na msafara wa watu 54 na watakaa huko kwa muda wa siku nne.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Meneja wa timu hiyo Faina Idarous Faina, alisema wakiwa mkoani huko wana mambo makuu matatu ambayo watayafanya.
Aliyataja mambo hayo kuwa moja ni kutembea katika sehemu mbali mbali, kucheza mechi za kirafiki pamoja na kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunaenda kwa ajili ya ziara ya kimichezo na tunatarajia kukaa huko kwa muda wa siku nne”, alisema.
Faina alisema wakiwa mkoani huko wamepanga kucheza mechi mbili za kirafiki moja watacheza na Polisi Veterani na mechi ya pili watajuwa watakapofika huko.
ZECO wamekuwa na utaratibu wa kufanya ziara za kimichezo kila ifikapo mwisho wa mwaka ambapo mwaka jana walifanya safari kama hiyo mkoani Arusha.