NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Umeme (ZECO) limewataka wananchi kutoa mashirikiano ya kutosha linapotokea tatizo la umeme katika utoaji wa taarifa kwa Shirika hilo, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma na kuepusha hitilafu zinazotokana na umeme.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Mawasiliano na huduma za wateja, Salum Abdallah Hassan, alisema mashirikiano ya baadhi ya wananchi katika utoaji wa taarifa za matatizo ya umeme ni madogo, jambo ambalo hupelekea usumbufu kwa watendaji, na kuchelewa kutatua tatizo kwa wakati.

Alitoa mfano kwa kusema, ili watendaji waweze kufika maeneo ya tatizo lazima nambari ya simu ya mtoa taarifa hiyo ipatikane muda wote, ili watendaji waweze kufika sehemu yenye tatizo kwa wakati kuweza kulipatia ufumbuzi na kuepusha hitilafu zinazotokana na umeme.

Lakini alisema jambo la kusikitisha ni kuwa, baadhi ya wananchi hutoa taarifa ya tatizo ila wakipigiwa simu kutopokea au hawapatikani kabisa jambo ambalo hupelekea usumbufu kwa watendaaji.

“Kwa mfano kuna tatizo la kuanguka nguzo ya umeme liliripotiwa kutoka Bambi Wilaya ya Kati, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa mafundi walikaribia eneo la tukio, lakini muhusika alietoa taarifa ambae alitakiwa kuwaelekeza kila akipigiwa simu hapatikani, hivyo suala kama hilo hupelekea usumbufu kwa watendaji wetu na kuchelewa kulitatua tatizo” alisema.

Alisema, ZECO ipo kwa ajili ya kutoa huduma iliyobora kwa wananchi wote, lakini changamoto huja kwa baadhi yao ambao hawatoi mashirikiano mazuri na kisha hulilaumu Shirika.

Hivyo aliwataka wananchi zinapotokea hitilafu za umeme kuwa na ushirikiano wa karibu na ZECO ili kuzitatua changamoto hizo na kuimarisha huduma hiyo nchini.