NA RAMADHANI ALI, MAELEZO

WAKALA wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA), imeteketeza tani 52 za mchele ulioingizwa nchini na mfanyabiashara Suleiman Abdalla tangu mwezi Machi mwaka jana.

Mchele huo uliokwishaharibika ulikuwa kwenye makontena mawili bandarini Malindi, ulitakiwa urejeshwe ulikonunuliwa ama uangamizwe kwa gharama za mfanyabiashara mwenyewe.

Mkurugenzi Idara za Huduma za Maabara wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar, Nadir Khatib Hassan, alisema mchele huo umeangamizwa jana katika jaa la Kibele.

Alifahamisha kuwa mafanyabiashara huyo ambaye aliuingiza mchezo huo nchini mnamo Machi 15 mwaka 2019 kutoka Pakistan, alikubali kugharamia zoezi la uangamizaji.

Alisema mchele huo ulikosa ubora kwa matumizi ya binadamu na ulikuwa na wadudu wengi tokea ulipoingizwa nchini.

Aliwashauri wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapokwenda kununua bidhaa nje na kufuatilia kwa karibu taratibu zote za usafirishaji ili kujiepusha na gharama zisizokuwa za lazima.

Hivi karibuni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla alifanya ziara katika bandari ya Malindi na kugundua uwepo wa kontena mbili zilizosheheni mchele huo.

Makamu huyo alitoa muda wa siku tatu kuondoshwa makontena hayo, huku akionya vikali kwamba Serikali haitosita kumfutia kibali mfanyabiashara  atakayejihusisha kuingiza bidhaa zilizopitwa na muda wa matumizi ama zilizokuwa hazina viwango.