NA KHAMISUU ABDALLAH

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), zimetakiwa kushirikiana kufanya ukaguzi wa bidhaa mara kwa mara kwa wafanyabiashara na maghala ya kuhifadhia bidhaa hasa za vyakula ili kuwaepusha wananchi kupata maradhi.

ZFDA

Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza, Wizara ya Afya, Omar Abdalla Ali, aliyasema hayo wakati akitoa elimu kwa waandishi wa habari juu ya lishe bora na lishe inayotakiwa kwa wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza yaliyofanyika katika ofisi za jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi hayo Mpendae.

Alisema ni jambo la msingi kwa taasisi hizo kufanya kazi pamoja ili kuwanusuru wananchi kupata maradhi kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuza vyakula vilivyopita muda bila ya kujali kuwa wanaharibu afya za walaji.

Alisema taasisi hizo zina jukumu kubwa la kuhakikisha vyakula vinavyouzwa vinakuwa na ubora na salama wakati wote kwa afya za wananchi.

Omar alisema wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakila vyakula vilivyopita muda hali ambayo inawasababishia kupata maradhi mbalimbali ikiwemo yasiyoambukiza kutokana na kutokuwa makini wakati wanapokwenda kufanya manunuzi.

Alisisitiza kuwa imefika wakati kwa taasisi hizo kuidhibiti hali hiyo ambayo imekuwa ikipoteza nguvu kazi ya taifa inayotegemewa katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar.

Alibainisha kuwa serikali kupitia wizara ya afya na jumuiya mbalimbali zimekuwa zikijitahidi kuelimisha jamii juu ya kujikinga na maradhi mbalimbali hasa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakichukua nafasi ya kwanza kwa vifo hapa Zanzibar.

Akizungumzia lishe, alisema changamoto kubwa kwa wanajamii ni kutokuwa na lishe isiyokamilika hali ambayo inapelekea kupata maradhi ikiwemo utapiamlo kwa watoto.

Alisema Zanzibar kuna matatizo mengi ya utapiamlo ambayo yanatokana na kuzidi au kupungua kwa virutubisho katika mlo wa mwanaadamu inayosabishwa na athari mbalimbali za kibinafsi, kijamii na kiuchumi.

Sambamba na hayo alisema pamoja na Zanzibar kuzungukwa na bahari lakini asilimia 99 ya wavuvi hawali samaki na badala yake huwauza kwa ajili ya kujipatia kipato.

“Zanzibar tumebarikiwa na vitoweo, matunda na mboga mboga lakini hatuna mazoea ya kula mlo kamili kutokana na kutojua lishe bora ndio inayotujenga mwili wetu na kutuepusha na maradhi mbalimbali,” alisema. 

Kwa upande wake Ofisa lishe wa kitengo hicho, Saleh Mohammed Haji, aliwasisitiza wananchi kujenga utamaduni wa kula vyakula bora ikiwemo mbogamboga na matunda na kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujiepusha na magonjwa mbalimbali.