Wajasiriamali Pemba wajengewa matumaini kibao

Dk. Mwinyi aahidi kupunguza kodi, lengo kuvutia uwekezaji 

NA RAJAB MKASABA

UJASIRIAMALI ni jambo kubwa duniani kote na limebadilisha maisha ya watu wengi kutoka katika hali ya umasikini na kuwafanya wawe na kipato kikubwa.

Kinachohitajika ni watu wawe mabunifu na majasiri wa kuzitumia fursa mbali mbali zilizomo katika jamii na mazingira inayoishi pamoja na kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa.

Mafanikio makubwa yamepatikana katika nchi zilizowajengea mazingira mazuri wananchi wake walioamua kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali.

Kadhalika dunia imeweka mifano  ya watu na taasisi zilizoanzishwa katika utaratibu wa ujasiriamali na hatimae kupiga hatua kubwa ya mafanikio ya kupigiwa mfano ambapo hata kwa upande wa Tanzania wapo wafanyabiashara wakubwa ambao chimbuko lao ni shughuli za ujasiriamali.

Wale wote waliofanikiwa katika shughuli za ujasiriamali, wametafsiri kwa vitendo dhana ya ujasiriamali kwamba ni kuwa na ujasiri katika kutafuta mali, kwa njia za halali.

Kwa mujibu wa Joseph Schumpeter ambaye ni mwana uchumi wa Australia, alisema kwamba “Ujasiriamali ni utaratibu na uendeshaji wa shughuli za kibiashara kwa ubunifu kwa lengo la kupata faida na kuwa tayari katika kukabiliana na hasara yoyote itakayojitokeza”.

Kwa mnasaba wa maoni ya mtaalamu huyo wa uchumi, mjasiriamali lazima awe na mipango madhubuti ya uendeshaji wa shughuli yake ya kiuchumi, awe na ubunifu kwa azma ya kupata faida ya biashara yake ikiwa ndio lengo kuu la kufanya biashara kwa mfanyabiashara yeyote hasa ikiaminika kwamba watu matajiri na maarufu duniani ikiwemo Zanzibar ni wajasiriamali.

Vi vyema wajasiriamali wakajifunza kutokana na historia za watu matajiri kama vile “Bill Gates”, Mwanzilishi wa Kampuni ya”Microsoft” kutoka Marekani, “Mark Zuckerberg”, ambaye ni Mjasiriamali wa mitandao na Mwanzilishi wa Kampuni na Mtandao wa “Facebook” na kwa Zanzibar ni Said Salim Bakhressa Mwanzilishi wa Kampuni ya “Azam Marine”.

Wajasiriamali wanaweza kujifunza mengi kutokana kwa Wajasiriamali hao ikiwemo historia zao na maendeleo waliyoyapata kwa ujasiri na ubunifu wao katika shughuli za ujasiriamali.

Kwa kutambua umuhimu wa Wajariamali Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni katika ziara yake ya siku mbili kisiwani pemba alikutana na makundi ya wajasiriamali wa Mikoa yote miwili ya Pemba akiwa na lengo la kutoa shukurani zake pamoja na kuwapongeza kwa kumuunga mkono na kumchagua kwa kura nyingi.

Pia, Rais Dk. Hussein Mwinyi alikutana na Wajasiriamali hao ikiwa ni miongoni mwa ahadi alizowaahidi wakati wa Kampeni kwamba mara tu atakapopata ridhaa ya wananchi basi atarudi kwa azma ya kwenda kuwashukuru na kuwapongeza.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliwaeleza wajasiriamali hao kwamba yuko tayari kutekeleza ahadi alizoziadi huku akisisitiza kwamba ataifanya Pemba kuwa sehemu maalum ya uwekezaji.

Katika maelezo yake wakati akizungumza na Wajasiriamali wa Mkoa wa Kusini Pemba kwenye ukumbi wa Skuli ya Fidel-Castro, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaweka mazingira mazuri kwenye vivutio vya uwekezaji ili iwe rahisi zaidi kuekeza katika kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa mbali na hatua hiyo, Serikali ya Awamu ya Nane itahakikisha inapunguza kodi kwa wawekezaji wote walioamua kuekeza katika kisiwa cha Pemba.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kuwa mazingira mazuri yatawekwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari, uwanja wa ndege, barabara sambamba na kuwa na maeneo maalum ya uwekezaji.

Alisisitiza kuwa hatu ya kuiweka Pemba kuwa ni sehemu maalum kutapelekea azma ya kutekeleza uwezekano wa kupatikana kwa ajira kati ya ajira 300,000 zilizoahidiwa katika Ilani ya Uachaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa wananchi wote kwa kufanya uchaguzi kwa amani sambamba na kuendelea kudumisha amani na umoja miongoni mwao.

Alitoa shukurani kwa vikundi vyote vya Wajasiriamali ambao aliwaahidi kukutana nao baada ya kumchagua na kumalizika kwa uchaguzi ambao umempa ushindi mkubwa na akaona haja ya kutekeleza ahadi yake hiyo.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza kwamba bila ya amani na umoja hakuna maendeleo na kuwataka wananchi wakiwemo wajasiriamali kujipongeza kwa hatua iliyofikiwa ya kudumisha amani iliyopo.

Aliongeza kuwa vyama vyote vya siasa hapa Zanzibar vimekubali kuwa kitu kimoja katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hivyo aliwataka wananchi kuweka tofauti zao za kiitikadi pembeni na kuwa kitu kimoja katika kuleta maendeleo.

Aliwataka wale wote ambao hawajaona umuhimu wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa watambue umuhimu wake na kuwataka wananchi wote kuunga mkono hatua hiyo ambayo itawaletea manufaa makubwa mbele yao.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliwaeleza wajasiriamali hao kwamba uchaguzi umekwisha na lililobaki mbele yao hivi sasa ni kushirikiana katika kuijenga nchi na kuwaletea wananchi maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba safu ya Mawaziri na Wakuu wa Mikoa ikotayari.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wote wa dini kwa kuliombea taifa na kuahidi kufanya kazi nao ili kuondoa changamoto zinazowakabili.

Pia, aliwaeleza wakulima atahakikisha kwamba changamoto zao walizomueleza wakati wa kampeni zinafanyiwa kazi kwa azma ya kuwaletea maendeleo na kuvitaka vikundi vyote kuwasilisha changamoto zao kwa Wakuu wa Mikoa na Mawaziri aliowateua.

Alieleza kwamba Mabenki mengi ambayo uongozi wake amekutana nao hivi karibuni yameahidi kushirikiana na Serikali anayoiongoza katika kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia masharti ya mikopo.

Alisema kwamba kinachohitajika hivi sasa kwa mabenki hayo ni kuwapatia wajasiriamali mikopo nafuu sambamba na kuwapa elimu ya kuwasaidia katika shughuli zao mara baada ya kupata mikopo hiyo.

Pamoja na hayo, alieleza kwamba tayari wapo wawekezaji ambao wameahidi kuja kuekeza katika sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi ambao wameahidi kujenga bandari,viwanda vya kusindika samaki, viwanda vya kutengeneza nyavu na vyenginevyo.

Alieleza kuwa hatua za makusudi pia, zitachukuliwa katika kuwasaidia wavuvi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ustadi zaidi ikiwa ni pamoja na kupata soko na kuondokana na uvuvi usio na tija.

Kwa upande wa Wajane, Rais Dk. Hussein alisema kuwa tayari Mama Mariam Mwinyi ameshaeleza utayari wake wa kuwa mlezi wa kundi hilo huku akiwataka wajasiriamali hao kukaa pamoja na kuorodhesha changamoto zao ili zipate kufanyiwa kazi.

Aidha, kwa upande wa wanamichezo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza juhudi zitakazochukuliwa katika suala zima la kupata udhamini ambalo ndio jambo muhimu katika kuimarisha michezo.

Aliongeza kuwa   anafahamu kwamba bado kuna changamoto katika michezo hasa katika mpira wa miguu ambapo katika chama cha mpira wa miguu cha Zanzibar (ZFF) chama hicho kina changamoto katika uongozi wake na kusisitiza kwamba kwa vile wanamichezo wapo, viwanja vipo cha muhimu hivi sasa ni kutafuta viongozi bora.

Alieleza azma ya kuondosha utitiri wa kodi kwa wajasiriamali wadogo wadogo sambamba na kuwapatia vitambulisho pamoja na kulipa kodi ndogo kwa mwaka ili waweze kufanya shughuli zao kwa wepesi zaidi.

Alieleza haja kwa wafanyabiashara kulipa kodi na Serikali itawawekea mazingira mazuri katika kuhakikisha wanafanyabiashara zao lakini cha muhimu ni kuja kulipa kodi zitakazowekwa japo kuwa ni ndogo.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza azma ya Serikali anayoiongoza katika kuwasaida watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na kuwataka viongozi aliowateua wanatekeleza majukumu yao kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu hasa ikizingatiwa kwamba wana mahitaji maalum.

Akiwa Mkoa wa Kaskazini Pemba Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa katika wakati wa Kampeni alikutana na makundi mbali mbali ambayo yalimpa changamoto zao na kuahidi kwamba changamoto hizo zote atazifanyia kazi ilimradi waweze kuongeza kipato chao.

Miogoni mwa makundi hayo ni wakulima ambapo kwa upande wao alisema kuwa atahakikisha kwamba changamoto zao walizomueleza wakati wa kampeni zinafanyiwa kazi kwa azma ya kuwaletea maendeleo na kuvitaka vikundi vyote kuwasilisha changamoto zao kwa Wakuu wa Mikoa na Mawaziri aliowateua ili zipate kufanyiwa kazi kwa haraka.

Pamoja na hayo, alieleza kwamba tayari wapo wawekezaji ambao wameahidi kuja kuekeza katika sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi ambao wameahidi kujenga bandari,viwanda vya kusindika samaki, viwanda vya kutengeneza nyavu na vyenginevyo.

Kwa maelezo yake atua za makusudi zitachukuliwa katika kuwasaidia wavuvi ili waondokane na uvuvi wa kizamani wa kutumia zana duni kwa kujenga viwanda vya kusindika samaki, bandari maalum pamoja na nyenzo kama vile nyavu ambazo zitatengenezwa hapa hapa Zanzibar.

Pia, alieleza kuwa wawekezaji wengi wameshaonesha nia ya kuekeza katika sekta ya uvuvi huku akisisitiza kwamba atahakikisha wakezaji wakubwa wanawasaidiwa wavuvi wadogo kwa kuwapatia soko la uhakika ambapo kwa upande wa Serikali itahakikisha inashirikiana nao ili iwasaidia wavuvi hao waweze kuondokana na umasikini.

Kwa upande wa Wajane, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari Mama Mariam Mwinyi ameshaeleza utayari wake wa kuwa mlezi wa kundi hilo ambapo pia, amemteua Mkuu wa Mkoa huo mwanamke ili kuhakikisha matatizo yao yanatatuliwa kwa haraka sambamba na maisha yao kuwa bora zaidi.

Pia, Ris Dk. Hussein Mwinyi aliwahakikishia wajasiriamali wadogo wadogo kwamba watajengewa  masoko ya kisasa, watapewa vitambulisho na kuweza  kulipa kodi mara moja kwa mwaka na kueleza kwamba linalofanywa na serikali hivi sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji ili wajasiriamali hao wapate kunufaika na biashara zao.

Alisema kuwa kwa upande wa wafugaji samaki juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha wanafanya shughuli zao vyema ikiwa ni pamoja na kupatiwa vifaranga vya samaki pamoja na kutafuta njia bora zaidi za ufugaji wa samaki sambamba na kuwasaidia wakulima wa mwani kulima mwani sambamba na kufuga majongoo ambavyo kwa pamoja vitainua kipato.

Aidha, alisema kuwa kila aina ya udhibiti utafanyika ili fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuweka kila aina ya udhibiti kwa lengo la kuwafikia wale wote wanaostahiki kuzipata fedha za mfuko huo.

Aliwataka wafanyakazi wa gereji kuorodhesha vifaa wanavyovitaka na baadae kumfikishia Mkuu wa Mkoa ili taratibu za kupata vifaa hivyo zifanyike katika kipindi kifupi kwani miongoni mwa changamoto walizozieleza wakati huo ilikuwa ni ukosefu wa dhana ama vifaa.

Kwa upande wa walemavu Rais Dk. Hussein alisema kuwa kundi hilo linahitaji msaada zaidi na kuahidi kila juhudi zitachukuliwa ili kundi hilo lisibaki nyuma.

Kwa upande wa kundi la vijana katika suala zima la ajira, alisema kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha viwanda vingi vinajegwa Unguja na Pemba ili vijana wengi waweze kupata ajira.

Alisema kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kila Wilaya iwe na eneo maalum la viwanda na miuondombinu iwe tayari kwani wawekezaji wapo na wako tayari hivyo, aliwataka vijana wawe tayati kufanya kazi.

Alisema kuwa miundombinu itajengwa ikiwemo bandari ili mizigo inayokwenda kisiwani humo iwe rahisi kufika pamoja na ujenzi barabara na miundombinu mengine.

Katika maelezo yake hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza juhudi zitakazochukuliwa katika kupambana na udhalilishaji katika jamii kwani ni jambo baya sana na kusisitiza kamwe serikali anayoiongoza haitokubali kushindwa na kadhia hiyo.

Aliwapongeza wajasiriamali hao kwa kumpa kura nyingi na jinsi walivyojitokeza kwa wingi katika mkutano huo huku akiwataka kumuombea dua yeye na watendaji wenzake, kuiombea dua nchi iendelee kuwa na amani na umoja uliopo ili kupata maendeleo zaidi.