NA HAFSA GOLO

MAMLAKA ya Usafiri Baharini (ZMA) imewataka wamiliki wa Boti na Meli kuhakikisha wanafata sheria za usafiri baharini hasa katika kipindi cha likizo, ili kulinda usalama wa abiria na mali zao.

Mkurugenzi Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Othman Said Othman, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Malindi mjini Unguja.

Alisema ni vyema wamiliki hao kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matakwa ya kisheria na kanuni zilizopo ikiwemo kuzingatia kuuza tiketi kwa mujibu wa idadi ya abiria iliyokubalika serikalini kufuatia chombo husika.

Aidha, alisema ZMA haitomvumilia mtu yoyote ambae atabainika kwenda kinyume na matakwa ya kisheria ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa chombo hicho kutofanya safari sambamba na kutozwa faini.

Alibainisha kwamba hatua hiyo iwe sambamba na uoneshaji wa vitambulisho wakati wa ununuzi watiketi na uingiaji wa chomba.

Alisema zoezi hilo liwe pamoja na mtoto mwenye umri kuanzia miaka sita hadi 11, anapaswa kukatiwa tiketi na kulipia nusu ya nauli ambapo miaka 12, na kuendelea anapaswa kukata tiketi na kulipia nauli kamili kama anavyolipa mtu mzima.

Alifahamisha kwa mujibu wa kanuni ya mwaka 2008, kuhusiana na vyombo vidogo na vyombo vilivyofanya safari katika mwambao, kufungu nambari 127 (5) na (6) kwamba mtoto mwenye umri kuanzia siku moja hadi miaka mitano hapaswi kukatiwa tiketi na kutozwa nauli bali mzazi wa mtoto huyo anatakiwa kumuandikisha jina lake katika fomu maalum kabla ya kuingia katika meli au boti.

Aidha alisema, mtoto mwenye umri kuanzia miaka sita hadi 11 anapaswa kukatiwa tiketi na kulipia nusu ya nauli na mtoto kuanzia miaka 12, na kuendelea anapaswa kukata tiketi na kulipia nauli kamili kama anavyolipa mtu mzima.