NA MWANDISHI WETU

BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB) imewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa mujibu wa taratibu na sheria za usimamizi wa kodi nchini. 

Kauli hiyo, ilitolewa na Ofisa Uhusiano wa bodi hiyo, Badria Attai Masoud, katika mkutano uliowashirikisha wafanyabiashara katika ukumbi wa Baraza la Mji Chake Chake Pemba.

Alisema wapo wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikiuka sheria za kodi, hali ambayo inapelekea mapato mengi ya serikali kupotea kiholela. 

Aliwasisitiza wafanyabiashara hao kuujua wajibu wao baada ya kusajiliwa kuwa walipa kodi rasmi na kuhakikisha wanatoa risiti kila wanapofanya mauzo yao,kujaza fomu za ritani na kufanya malipo kwa wakati kwa bodi hiyo. 

Ofisa Badria, aliwashauri wafanyabiashara ambao bado hawajasajiliwa na bodi  hiyo, kujisajili mara moja ili watambulike rasmi kuwa walipakodi halali na kujiepusha na matatizo yasiyokuwa ya lazima ikiwemo kufungiwa biashara zao.

Alisema kufanya biashara bila kusajiliwa ni makosa makubwa kisheria na serikali haipo tayari kuwafumbia macho wafanyabiashara wote ambao wanakwepa wajibu wao kulipa kodi ambayo inategemewa kwa ajili ya maendeleo ya nchi. 

Kwa upande wake Ofisa Elimu wa bodi hiyo, Raya Suleiman Abdalla, aliwaomba wafanyabiashara kuhudhuria katika mikutano na semina mbali mbali ambazo zinaratibiwa na ZRB, kwani zina lengo la kuwapa elimu na kujua wajibu wao katika kodi.