ZSTC ni zao la Mapinduzi matukufu ya 1964

  • Karafuu bado ni zao la taifa Zanzibar
  • Uzalishaji, kipato cha wakulima chaongezeka

NA ALI MOHAMED, ZSTC

KWA mujibu wa Sheria ya Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar Namba. 11 ya 2011 Kazi za Shirika la ZSTC ni kushughulikia Maendeleo ya Sekta ya Karafuu, kununua na kuuza karafuu na mazao mengine ya kilimo. Kufanya usarifu na kuongeza thamani ya karafuu na Mazao mengine ya kilimo.

Kazi nyengine ni kukusanya, kuchambua, kusambaza habari na utaalamu juu ya zao la karafuu. Kutunza taarifa na takwimu zinazohusiana na karafuu na mazao mengine ya kilimo. Kuweka bei za ununuzi wa karafuu pamoja na mazao mengine ya kilimo toka kwa wakulima na Kuamua ubora wa karafuu pamoja na mazao mengine ya kilimo.

Katika kipindi hichi tukiazimisha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 tutaangalia Maendeleo na mafanikio ya Sekta ya Zao la Karafuu na Biashara.

Historia inaonyesha kuwa ZSTC ni miongoni mwa mashirika ya mwanzo kuanzishwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, hivyo historia ya ZSTC na Maendeleo ya Sekta ya Zao la Karafuu inakwenda sambamba na historia ya Zanzibar kulingana na awamu, mabadiliko na mageuzi yanayotokea.

Baada ya Mapinduzi ya Januari 12/1964, Rais wa kwanza Hayati Abeid Amani Karume alikuta hazina imenenepa na akaiacha bado nono baada ya kuyatumia mapato yaliyotokana na zao la karafuu kuijenga Zanzibar. Wakati huo Zanzibar ilikuwa ikikusanya hadi tani 71,873 za karafuu kwa msimu.

Mapato hayo yalimpa uwezo mkubwa Mzee Karume kutamba katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa uchumi imara.

Serikali ya awamu ya pili chini ya uongozi wa Marehemu Mzee Aboud Jumbe Mwinyi iliendeleza jitihada za Uimarishaji na ulinzi wa zao la karafuu.

Katika kipindi chake, Mzee Jumbe alihamasisha uatikaji wa miche mipya iliyotokana na uchanganyaji wa mbegu na kutoa mikarafuu iliyoanza kuzaa ikiwa na umri mdogo kuliko ilivyozoeleka pamoja na kutoa dawa ya kutibu mikarafuu ambayo wakati huo ilikuwa inazeeka kwa kasi.

Katika mwaka 2011 zilifanyika tafiti juu ya namna ya kuimarisha Sekta ya Karafuu, kuliimarisha Shirika la ZSTC pamoja na kuzifanyia kazi changamoto za wakulima ikiwemo bei. Serikali ilidhamiria kuzifanyia kazi changamoto katika sekta ya zao la karafuu ambapo ilianzisha na kutekeleza Mkakati Maalumu wa miaka kumi (10) 2011/2021 ya Mageuzi katika Sekta ya Karafuu.

Utekelezaji wake ulianza kwa kulifanyia Mageuzi makubwa Shirika la ZSTC ikiwemo kubadilisha Mfumo wa uendeshaji wa Shirika, kubadilisha sera ya malipo kwa mkulima wa karafuu na kupunguza idadi ya wafanyakazi na kuajiri wengine wenye sifa kulingana na mahaitaji ya mageuzi.

Utekelezaji wa mkakati huo ulifanikiwa zaidi pale Serikali ilipopitisha Sheria mbili, moja ni sheria ya ZSTC Na. 11 ya mwaka 2011 inayoipa Mamlaka na uwezo mkubwa Shirika la ZSTC kulisimamia, kulihudumia, kuliimarisha na kuhakikisha zao la Karafuu linakuwa endelevu kwa maslahi ya wakulima, wananchi na Taifa kwa ujumla.

Na sheria ya pili ni sheria ya Maendeleo ya Karafuu Na. 2 ya Mwaka 2014 pamoja na Kanuni zake. Kupitia Sheria hii ya Maendeleo ya Karafuu chini ya kifungu Na. 4 (1), Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ulianzishwa.

Sera ya kuwapa wakulima asilimia 80 ya bei ya kuuzia katika soko la dunia imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa ambapo hivi sasa mkulima wa zao la karafuu analipwa wastani wa shilingi 14,000 kwa kilo moja ya karafuu kavu, kutokana na bei hii wakulima wananufaika sana na kilimo cha karafuu, wemeongeza ari ya kulihudumia zao la karafuu, wanauza karafuu zote kwa ZSTC na magendo yamepungua sana.

Katika kipindi cha miaka kumi 2011-2021 cha utekelezaji wa mageuzi uzalishaji na usafirishaji wa zao la karafuu umeimarika sana. Katika kipindi cha mwaka 2011/2012 hadi Mwezi Disemba 2020 jumla ya tani 36,094.68 za karafuu kavu zimenunuliwa kutoka kwa wakulima, karafuu hizo zina thamani ya shilingi 507.236 bilioni.

Kwa mujibu wa watumiaji wa karafuu dunia, karafuu ya Zanzibar ni bora kuliko kafuu nyengine kutoka nchi wazalishaji, Serikali za awamu zote tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 zimefanya jitihada za kulinda ubora huo kwa nguvu zote.

Shirika la ZSTC limeendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna ya kulinda ubora wa zao la karafuu. Mashine tano (5) za kusafisha karafuu kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa mauzo na mashine sita (6) za kupimia kiwango cha unyevu wa karafuu (moisture content) zimenunuliwa na kutumika.

Katika uimarishaji wa sekta ya karafuu Serikali katika awamu zote zimewapa kipaombele zaidi wakulima wa zao la karafuu kwa nia ya kuwanufaisha zaidi na kuongeza ari ya uzalishaji kinyume na ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ambapo wachache ndio walioneemeka zaidi na zao hilo.

Wakulima wa zao la karafuu hivi sasa wananufaika na mpango wa Bima ambapo wanaopata ajali wakati wa uchumaji karafuu wanafidiwa lengo likiwa kuwajengea ari na moyo wananchi kushiriki shughuli za uchumaji.

Kuanzia mwaka 2015/16, baada ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu hadi mwaka 2018/19 wakulima waliopata ajali wakati wakichuma karafuu ni 403. Wakulima 339 wamelipwa jumla ya TZS 266.1 milioni tokea kuanzishwa kwa bima hiyo.

Aidha, wakulima wanapatiwa miche ya mikarafuu bila ya malipo, mwaka 2000 lengo lilikuwa kuotesha na kupanda miche 500,000 kwa mwaka na mwaka 2014 lengo likaongezwa hadi miche 1,000,000, kwa mwaka.

Juhudi hizo zimeleta ufanisi ambapo idadi ya mikarafuu mipya imeongezeka, kwa mujibu wa tathmini ya miti ya mikarafuu jumla ya miche 3,465,034 imepandwa ambapo baadhi ya mikarafuu hiyo imeanza kuzaa.

Serikali imekuwa ikiwawezesha wakulima kujiandaa katika uchumaji wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar kupitia mikopo isiyokuwa na riba. Kuanzia mwaka 2011/2012 hadi mwaka 2018/19, jumla ya shilingi 1,286,850,000 zimetolewa kwa wakulima.

Shirika la ZSTC limeamua kufanya usajili wa mashamba, wakulima na wadau wengine muhimu wa zao la karafuu ili kusaidia katika kufanya makisio ya karafuu kwa usahihi zaidi pamoja na kupunguza wizi wa karafuu mashambani.

Usajili ulianza mwaka 2016 ambapo jumla ya wakulima 4,127 na wanaokodi 507 wamesajiliwa, mashamba ya watu binafsi 2,431, ya serikali 13 na mashamba ya eka 2,048 yamesajiliwa na wakulima 1580 washapewa vitambulisho.

Shirika la ZSTC limeendelea kuimarisha vituo vya ununuzi wa karafuu na makonyo ambapo vituo vimekarabatiwa na vyengine kujengwa upya, vituo hivyo vinaendana na hadhi na thamani ya zao la karafuu. Kutokana na ubora wa vituo hivyo hutumiwa na wananchi kwa shughuli zao za kijamii wakati msimu wa manunuzi unapomaliza.

Kiwanda cha mafuta ya Makonyo kilichopo Wawi Chake chake Pemba ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ya mwaka 1964, hivyo Shirika la ZSTC limeendelea kukifanyia matengenezo kiwanda hicho kwa kufunga mitambo mipya ya kupoozea mvuke, mashine ya kuchemshia makonyo (boiler) mpya yenye uwezo wa kuzalisha mvuke tani nane (8) kwa saa pamoja na kufunga vinu vipya vitano (5) vya kusindika majani ya mkaratusi.

Bidhaa za karafuu

Shirika la ZSTC imedhamiria kuwainua zaidi wakulima kwa kubuni na kutekeleza mipango ya kuyaongezea thamani mazao ya viungo ya Zanzibar ikiwemo Karafuu, Pilipili hoho, Pilipili manga na Mdalasini.

Hivi sasa tayari karafuu pamoja na viungo hivyo vina utambulisho maalum katika soko la dunia. imeimarisha kilimo hai ambapo jumla ya wakulima 100 wamepatiwa elimu juu ya jinsi ya kutayarisha mashamba, uhifadhi wa mazao baada ya kuvunwa pamoja na zana za kutumia kwa ajili ya kilimo hicho. Mazao ya kilimo hai yana thamani kubwa katika soko la nchi za Marekani na Ulaya.

Katika kipindi cha miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar kuna mengi ya kujivunia katika sekta ya zao la karafuu, Maendeleo ya Shirika la ZSTC na biashara kwa jumla huwenda muda usitoshe kuyasimulia yote.

“Karafuu ni uhai’ Karafuu kwa Maendeleo ya Zanzibar”