Utawala bora nguzo imara kufikia maendeleo

Rais Mwinyi ataka mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, kutowajibika

KAUTHAR ABDALLA

JANA Zanzibar iliadhimisha mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo yalikuwa ni ya kufana.

Kilele hicho kilikuwa ni azma katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu bure, afya bure pamoja na ardhi, mambo ambayo kabla ya Mapinduzi yalitolewa kwa ubaguzi.

Zanzibar ina historia kubwa katika kupambana na juhudi za kuhakikisha wananchi wake wanapata haki zao za msingi pamoja na kuwepo kwa utawala bora tokea kupatikana kwa uhuru wa Zanzibar.

Hatua hizo zimeipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi sasa kuendeleza haki za binaadamu sambamba na utawala bora na kupelekea kuipaisha Zanzibar kidemokrasia.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiko tayari kukiuka vifungu vya Katiba na Sheria zilizopo katika suala zima la haki za binaadamu na utawala bora na badala yake itaendelea kufuata taratibu zilizopo kwa ajili ya manufaa ya nchi na wananchi wake wote.

Zanzibar haina utamaduni wa kuvunja haki za binaadamu na badala yake imekuwa ni nchi yenye kufuata na kutekeleza haki za binaadamu, utawala bora pamoja na demokrasia kwa vitendo.

Serikali ya awamu ya saba iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Dk. Ali Mohammed Shein iliona kwamba,maendeleo, amani na utulivu ni dhana zenye maana zinazotegemeana.

Ili kuwe na maendeleo kunahitajika kuwe na amani na utulivu na kwa upande mwengine, amani na utulivu haiwezi kupatikana ikiwa hakuna maendeleo ni kama uhusiano wa kuku na yai.

Katika hutuba yake ya kufungua baraza la tisa la wawakilishi Dk. Shein amesema maendeleo katika nyanja mbali mbali za maisha ndiyo yanayowaletea wananchi utulivu, na utulivu ndio unaoleta amani.

Alisema wananchi wanaokabiliana na dhiki za maisha hasa katika kupata huduma muhimu za kuyamudu maisha yao, mwishowe hujenga hasira, ambayo huzaa chuki miongoni mwao na kusababisha matendo maovu yanayopelekea kuvunjika kwa amani.

Alisema ili uwiano mzuri upatikane baina ya amani, utulivu na maendeleo ni lazima tuhakikishe kwamba Serikali inaongozwa katika misingi ya utawala bora.

Aidha amesema miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili.

Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi imeahidi kukabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo.

Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali.

Umuhimu wa utawala bora umeelezwa kwa ufasaha na kwa ufupi mno na Profesa na Mwanasaikolojia, Amit Abraham pale aliposema, inapaswa pawe na itikadi moja tu ya kisiasa, ambayo  ni utawala bora.

Katika kuhakikisha kuwepo kwa Utawala Bora, Serikali ilianzisha Taasisi mbali mbali za kuusimamia mfumo huo.

Katika kupambana na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma,Serikali ya  Mapinduzi ya Awamu ya Saba, imeanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na  Uhujumu wa  Uchumi Zanzibar (ZAECA) chini ya Sheria  Nambari 1 ya mwaka 2012.

Jumla ya tuhuma 950 za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma zimefikishwa na Taasisi hii tangu ilipoanzishwa.

Tuhuma 751 kati ya hizo, bado zinachunguzwa na nyengine zimeshatolewa maamuzi.

Vile vile, Mamlaka imefanikiwa kuokoa na kurejesha Serikalini fedha na mali zenye thamani ya shilingi milioni 411.90 tangu kuanzishwa kwake.

Kadhalika,Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Nam 8 ya 2015.

Katika hutuba yake ya kufungua baraza la kumi la wawakilishi Rais wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi aliwaambia wajumbe kwamba,suala la maadili ni muhimu kwa viongozi kwa kuzingatia maadili na kuwa wakweli, ili wajenge imani kwa wananchi wanaowaongoza na kujiamini wao wenyewe wanapoikabili jamii kwa masuala mbali mbali.

Dk.Mwinyi amesema wanapokuwa na tabia zisizopendeza kwenye jamii, huwa wanakosa kujiamini na mara nyingi huishi katika maisha ya wasi wasi. 

Rais amewasisitiza viongozi wenzake lazima wawe na tabia njema na waendelee kushikamana na maadili ya kazi na katika jamii wanazoishi.

Alisema Taasisi hizo ni muhimu katika kuimarisha maadili ya viongozi na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. 

Wote wanatekeleza vizuri,matakwa ya sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma na waendelee kutimiza wajibu wao na kujipamba na sifa za uongozi bora unaofuata maadili.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) imeanzishwa kwa Sheria Namba 2 ya mwaka 2010.

Alisema Serikali imeimarisha mfumo wa haki jinai kwa kuiwezesha ofisi hio kusimamia utaratibu wa upelelezi na utaratibu maalumu wa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji pamoja na dawa za kulevya.

Hali hii imepelekea kupunguza kwa kiasi kikubwa mrundikano wa kesi mahakamani. Ofisi hii, inasimamia kituo cha Mafunzo ya Sheria na Utafiti ambapo jumla ya washiriki 513 wamehitimu katika kituo hicho.

Kadhalika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, katika kipindi hiki cha miaka kumi imeimarishwa na kujengewa mazingira ya kuiwezesha kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi. 

Ripoti za uchunguzi na ukaguzi wa hesabu za Serikali zinawasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa wakati kwa mujibu wa ibara ya 112(5) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984. 

Kwa kipindi kirefu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilikuwa ikifanya kazi zake kwa kuzingatia masharti ya Katiba na yaliyomo katika sheria mbali mbali. 

Mnamo mwaka 2013, Serikali ilianzisha rasmi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kisheria, kwa Sheria Namba 6 ya mwaka 2013. 

Ofisi  hii imetekeleza vyema majukumu yake ikiwemo kuzisimamia kesi za Serikali, kuandaa Miswada ya Sheria na kutoa ushauri wa kisheria kwa Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiko tayari kukeuka vifungu vya Katiba na Sheria zilizopo katika suala zima la haki za binaadamu na utawala bora na badala yake itaendelea kufuata taratibu zilizopo kwa ajili ya manufaa ya nchi na wananchi wake wote.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta za elimu na afya hiyo ni kutokana na kutekeleza vyema lengo na azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi ambazo hapo mwanzo hawakuzipata.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

CAP

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akitoa Hotuba yake kwa Viongozi mbali mbali katika   Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar